Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kuwa chaguzi nyingi za amani na makubaliano zinazofanyika barani Afrika kwasasa ni ishara ya kukomaa kwa Demokrasia.
Ameyasema hayo jijini Addis Ababa nchini Ethiopia wakati wa kilele cha mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo wakuu wa mataifa 55 wanachama wamekutana.
“Huu ndiyo wakati ambao upepo wa matumaini unavuma kote Afrika. tumeshuhudia maridhiano kati ya Ethiopia na Eritrea, tumeona makubaliano ya amani nchini Sudan Kusini na CAR (Jamhuri ya Afrika ya Kati),” amesema Guterres.
Aidha, amesema kuwa kwasasa wanashirikiana kuona namna ya kutafuta suluhisho la vurugu nchini Libya, huku akitolea mifano ya nchi za Afrika zilizofanya uchaguzi wake kwa amani ambazo ni Madagascar, DRC na Mali ambapo watu walikuwa wanatabiri utasababisha majanga na vurugu.
Ethiopia na Eritrea mwaka uliopita zilihitimisha vita baridi vilivyodumu kwa miongo miwili, huku Sudan Kusini ikijaribu kutekeleza makubaliano ya karibuni zaidi katika orodha ndefu ya makubaliano ya amani ya kukomesha mgogoro wa umwagaji damu uliodumu kwa miaka mitano.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilifikia makubaliano ya amani kati ya serikali na makundi 14 ya wanamgambo, na kuimarisha matumaini ya kukomesha mgogoro ulioikumba nchi hiyo tangu 2012, na kuzusha mzozo uliosababisha vifo vya maelfu ya watu na zaidi ya milioni kupoteza makazi yao.