Siku kadhaa baada ya kuthibitika wameondoka Young Africans, wakongwe Kelvin Yondani na Juma Abdul, wameanza kuzichonganisha Namungo FC na Gwambia FC ambazo msimu ujao zitakua sehemu ya Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wawili hao waliondoka Young African, baada ya kushindwa kuafiki baadhi ya utaratibu wa kusaini mikataba mipya, huku ikidaiwa uongozi wa klabu hiyo ulikua tayari kuwasainisha pasina kuwapa fedha za usajili, na kuendelea kuwalipa mishahara kama ilivyokua kwenye mikataba yao iliyomalizika.
Klabu ya Namungo FC ambayo msimu wa 2019/20 ilionkena kuwa moto wa kuotea mbali, inahusihwa na mpango wa kuhitaji huduma ya wakongwe hao, hasa kwenye michuano ya kimataifa.
Taarifa ya klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Ruangwa mkoani Lindi imeeleza kuwa, Namungo FC itasajili wachezaji wanane kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa, huku Yondani na Juma wakihusishwa kwenye mpango huo.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Zidadu, amesema wanatarajia kusajili wachezaji wanane kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika barani Afrika (CAF) wenye uwezo wa kuwasaidia kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
“Tumeshaanza mchakato wa usajili kwa wachezaji wapya ili kuongeza nguvu kikosini, lakini tunawaongezea mikataba wachezaji wa zamani ambao muda wao wa mikataba umemalizika, lengo ni kufanya vema kwenye michuano ya Ligi Kuu na kimataifa kwa sababu ikumbukwe kuwa tunawakilisha nchi, hivyo usajili ni lazima uwe wa kimataifa kwa wachezaji wa nje na wa ndani wawe wazuri na wazoefu, kwa hiyo mashabiki wetu watulie, wasihofu kuhusu usajili,” amesema mwenyekiti huyo.
Ingawa hakutaja ni wachezaji gani ambao wameanza mchakato wa kuwasajili, lakini habari za ndani zinaeleza kuwa klabu hiyo iko kwenye mazungumzo na Yondani na Abdul ambao hivi karibuni waliachwa na klabu ya Young Africans baada ya kutoafikiana kwenye mchakato wa kuongeza mkataba.
Hata hivyo, zipo taarifa kuwa wachezaji hao pia wanawaniwa na Gwambina FC ambao nao wameonyesha nia ya kuwasajili na mazungumzo kati ya pande mbili yanaendelea.