Mchezo wa Draft mashindano ya Michezo ya Mei Mosi 2023 umefikia tamati Aprili 27, 2023 kwa kupata mabingwa wa mchezo huo kwa wanaume na wanawake mkoani Morogoro.
Kwa upande wa wanaume bingwa wa mchezo wa draft kwenye mashindano hayo ni Salum Simba kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, mshindi wa pili ni Mussa Chilendu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi) na mshindi wa tatu ni Rashid
Mwichande kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati kwa upande wa wanawake bingwa wa mchezo huo ni Skitu Chande kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, mshindi wa pili ni Sophia Kambaya kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) na mshindi wa tatu ni Celine Simon kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi).
Kwa upande wa mchezo wa netiboli, mabingwa watetezi wa mchezo huo ambao ni timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imeingia fainali baada ya kuwafunga timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) kwa magoli 74-32 katika mchezo wa nusu fainali wa michuano ya kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, mkoani hapa.
Katika mchezo huo uliochezwa kwa robo nne, washindi waliongoza robo ya kwanza kwa 15-10; na hadi mapumziko ilikuwa 36-15; na robo ya tatu ni 52-22.
Katika mchezo mwingine uliokuwa mkali timu ya Ofisi ya Rais Ikulu waliwachapa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa magoli 26-25, hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 19-18 kwa hatua hiyo, imu ya Sekta ya Uchukuzi itakutana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga kwa kuwania ushindi wa tatu.
Katika mchezo wa mpira wa wavu wanaume timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii waliwafunga RAS Dodoma kwa seti 2-0 uliofanyika kwenye uwanja wa Bwalo la Umwema, huku Sekta ya Uchukuzi walipata ushindi wa chee dhidi ya Morogoro DC ambao hawakuonekana uwanjani.
Aidha, katika mchezo wa mpira wa miguu hatua ya nusu fainali, timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wametinga fainali kwa kuwafunga timu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa magoli 2-1 na timu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI imeinga fainali kwa kuwafunga timu ya Mahakama Tanzania kwa magoli 3-2.
Kwa upande wa mchezo wa kamba wanaume, timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi) imeingia fainali kwa kuwavuta timu ya Ofisi ya Rais Ikulu kwa mivuto 2-0 na kuungana na timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kivuta timu ya Mahakama kwa mivuto 2-0 wakati kwa upande wa timu za wanawake, timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi) wamewavuta timu ya Wizara ya Afya kwa mivuto 2-0 na timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wamewavuta timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mivuto 2-0.
Michezo hiyo ya Mei Mosi 2023 inayofanyika mkoani Morogoro inatarajiwa kufikia tamati Aprili 29, 2023 kwa fainali za michezo ya mpira wa miguu, netiboli na mchezo wa kamba wanaume na wanawake.