Simba imefanikiwa kuifunga Stand United mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara, mchezo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga, baada ya matokeo hayo Simba imefanikiwa kushika usukani wa ligi hiyo licha ya kulingana pointi na Mtibwa Sugar.
Kufuatia ushindi huo, afisa Habari wa Simba, Haji Manara ametupa kijembe kwa wapinzani wao kwa kuwaambia wanapambana na hali zao.
“Sasa hivi tunaongoza ligi kwa wastani mzuri wa mabao ambayo pengine ukihesabu timu tano au nne zinazotufuata ukijumlisha mabao yao ndiyo unapata mabao yetu.
“Kwa hiyo lazima tuwapongeze wachezaji wetu kwa kazi kubwa waliofanya, nadhani unaona wenzetu wanavyopambana na hali zao,” alisema Haji Manara.
Aidha, Manara pia ametoa tahadhari kwa Bodi ya Ligi na TFF kuhusu maamuzi yanayotolewa na baadhi ya waamuzi huku akimlalamikia mwamuzi kukataa bao la Laudit Mavugo kwamba mshambuliaji huyo alifunga bao akiwa katika nafasi ya kuotea.
Licha ya kuwa hajataja timu nyingine zaidi ya Simba katika maelezo yake lakini ni wazi dongo hilo linaenda kwa Yanga ambao ndiyo wapinzani wakubwa wa Simba.