Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam imeutaka upande wa mashtaka kuieleza mahakama kama hawana mashahidi katika kesi ya kutoa Lugha chafu dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, inayomkabili mbunge wa Kawe kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Halima Mdee
Hatua hiyo imekuja mara baada ya Wakili wa Serikali, Sylivia Mitando kudai mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba kuwa shahidi waliokuwa wanamtegemea kutoa taarifa kuwa anaumwa.
”Nilijitahidi kuwasiliana na shahidi lakini aliniambia kuwa anaumwa kuwa hawezi kufika kwasababu anaumwa, hivyo naiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kusikilizwa,”amesema wakili Mitando
Hakimu Simba amesema kuwa kesi hiyo ipo mahakamani hapo tangu Julai 10, 2017 ambapo kwasasa inatimiza miaka miwili na mashahidi waliotoa ushahidi ni watatu, hivyo amewaomba wafunge ushahidi kama wamemaliza.
”Natoa nafasi nyingine ya mwisho, leteni mashahidi waje kutoa ushahidi hadi sasa waliotoa ushahidi ni watatu tu, sipendi ifike Oktoba mwaka huu, nataka nilitolee maamuzi,”amesema Hakimu Simba