Serikali kupitia wizara ya afya inaendelea na taratibu za kisayansi na kitaalamu ili kujiridhisha na ugonjwa wa mlipuko ulioua watu watano kwa dalili zinazofanana mkoani Kagera na wakijilidhisha watatoa majibu ya ugonjwa huo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa afya daktari Godwin Molel wakati akizungumza na waandishi wa habari alipowasili mjini Bukoba
Amesema “kwa wakati huu tumejipanga kuhakikisha kuna fedha, vifaa vya kutosha kuwakinga watumishi, kuna magari ya kutosha lakini pia wizara imekuja na vifaa, kikubwa ni kwamba kuendelea kuwahasa wananchi kuzingatia maelekezo yote ambayo wataalam wa afya wanatoa”.
Naibu huyo wa wizara ya afya ameongeza kuwa kuna hatua mbali mbali inabidi zichukuliwe kabla ya kutangaza majibu ya ugonjwa huo.
Naye mganga mkuu wa hospitali ya rufaa mkoa wa Kagera Dr. Issessanda Kaniki wakati akizungumzia kuhusu taratibu zilizochukuliwa ili kuhifadhi miili ya watu watano waliofariki kwa dalili za ugonjwa huo, amesema kuwa miili hiyo imezikwa katika maeneo ya vijijini kwao kwa kufuata taratibu zinazobidi zichukuliwe wakati wa mazishi ya watu waliofariki kwa magonjwa ya mlipuko.
“Miili ilihifadhiwa kwa kufata taratibu za afya, watumishi wetu wakiwa wamevalia mavazi rasmi lakini pia vifaa vyote rasmi kwa ajili ya wahisiwa wa magonjwa ya mlipuko. Hata ambao tumewazika nao taratibu zimefatwa na wananchi wametusaidia sana”.
Naibu waziri wa afya Daktari Godwin Mollel pia amesema mpaka sasa hakuna wagonjwa walioongezeka wala vifo na ameendelea kuwataka wananchi kuzidi kuchukua tahadhali ya magonjwa ya mlipuko.