Kufuatia kauli ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kusema yupo katika mjadala ili mwanaye ambaye ni Jenerali wa Jeshi Muhoozi Kainerugaba ajiondoe kwenye mtandao wa Twitter, mtoto huyo ameibuka na kujibu kuwa hakuna wa kumzuia kwani yeye ni mtu mzima.
Muhoozi amekataa kupigwa marufuku kwenye Twitter ikiwa siku moja baada ya baba yake, Rais Museveni, kusema atamkataza kutoa maoni yake kuhusu masuala ya Serikali kwenye mtandao huo.
Hatua ya Museveni kuingilia kati suala hilo, ilifuatia ujumbe tata wa Jenerali Kainerugaba wiki mbili zilizopita ambapo alitishia kuivamia nchi jirani ya Kenya, na hivyo kusababisha kuomba radhi kwa umma na mikutano ya kidiplomasia ili kuthibitisha uhusiano huo.
Kama ishara ya kuhakikisha tukio kama hilo haliendelei, Rais Museveni pia Jumatatu (Oktoba 17, 2022) alisema jenerali huyo ataepuka kuzungumza kuhusu nchi nyingine na siasa za upendeleo za Uganda kwenye mtandao wa Twitter.
Kuhusu madai ya kumtaka Museveni ampigwe mwanaye marufuku kwenye mtandao wa kijamii, Jenerali Kainerugaba amesema ” mimi ni mtu mzima na hakuna mtu angenipiga marufuku kwa chochote,” tweet ambayo inajiri siku chache baada ya Muhoozi mwenyewe kuomba msamaha kwa umma kutokana na matamshi yake.
Jenerali Kainerugaba, anajulikana kwa tweet zake zenye utata, zikiwemo za kuunga mkono uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na waasi wa Tigrayan wanaopigana na serikali ya Ethiopia na zile za kufedhehesha kama ya kusema ataichukua Nairobi si chini ya siku 14 yeye na Jeshi lake.