Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ameielekeza Halmashauri ya Kondoa mkoani Dodoma kumaliza miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ifikapo Julai 15, 2023.
Ametoa maelekezo hayo leo Mei 09, 2023 alipofanya ziara ya kukagua shughuli za Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) na kubaini kutokamilika kwa uchimbaji wa visima virefu viwili kati ya nane vya maji safi wakati tayari Serikali ilishapeleka fedha.
Dkt. Jafo alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu miradi na kutoa fedha ili wataalamu wa halmashauri watekeleze miradi lakini wameonesha kusuasua na hivyo wananchi kukosa huduma ya maji.
Alisema suala mazingira ni mtambuka hivyo lengo la mradi ni kuwanufaisha wananchi ili waweze kufanya shughuli mbadala za kiuchumi na kuachana na shughuli zinaazohusiana na uharibifu wa mazingira.