Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amezitaka Halmashauri na mamlaka za Serikali za Mikoa kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan la kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji, ili kukuza sekta hiyo na kuepusha migogoro ya matumizi ya ardhi.
Waziri Ndaki, ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro, na kuzungumza na wakulima na wafugaji katika vijiji vya Tanga na Njiwa, ambapo amesema serikali ina nia nzuri ya kuendeleza Sekta ya Mifugo na kuwataka wafugaji kutolisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.
Amesema, “Halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa zinapaswa kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji, kama yapo maeneo yaliyotengwa na kijiji au kata kwa ajili ya malisho hayo maeneo yasajiliwe rasmi kuzuia migogoro.”
Aidha, ameongeza kuwa taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zinazonesha uwepo wa vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili 2022, kutishia upungufu wa malisho ya mifugo na maji, hivyo Wizara inatoa tahadhari juu ya suala hilo.
“Tuchukue tahadhari ya kuvuna mifugo yetu tusije kukutana na ukame halafu tukaanza kulalamika mifugo imeanza kuwa dhaifu au kufa huku tulikuwa tukijua ni vizuri ukapunguza kwa kuvuna mifugo yako na kubaki na ile itakayotosheleza malisho uliyonayo pamoja na maji,” amesisitiza Waziri Ndaki
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mathayo Maselle amesema skimu ya umwagiliaji iliyopo Kijiji cha Njiwa na Itete ambayo imetengwa maalum, kwa ajili ya kilimo imekuwa na changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika eneo hilo, imekuwa ikisababisha migogoro.
Akijibu changamoto hiyo, Waziri Ndaki ameutaka uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na wakulima na wafugaji kutengeneza mfereji utakaosafirisha maji kutoka kwenye skimu hiyo hadi eneo lingine watakalolitenga kwa ajili ya matumizi mbalimbali, badala ya mifugo hiyo kupita kwenye mashamba ya wakulima kufuata maji.
Baadhi ya wananchi katika eneo hilo, wametoa maoni yao ikiwemo namna ya utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji, na kuomba uwepo wa mpaka maalum wa skimu ya umwagiliaji ya vijiji vya Itete na Njiwa, ili wakulima waweze kufanya shughuli zao na wafugaji wapate huduma ya maji bila kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.