Mkenya Alfred Juma Ayora, ameiandikia Mahakama ya Juu na Jaji Mkuu Martha Koome kusitisha kuapishwa kwa Rais Mteule William Ruto, katika kile kinachoonekana kuwa ni ‘ombi’ la kwanza katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya uchaguzi wa Urais.

Hata hivyo, barua hiyo haikukubaliwa kwa sababu ya kutofuata sheria ambazo zinahitaji kuwasilishwa kwa ombi rasmi na sio barua, kutokana na Ayora kuwasilisha barua yenye aya mbili akiomba maagizo ya kubatilisha uchaguzi wa Ruto na Naibu Rais mteule Rigathi Gachagua, ambapo Mahakama ilimshauri aandae ombi lake.

Kesi ya uchaguzi wa urais, inapaswa kuwasilishwa katika Mahakama ya Juu ndani ya siku saba baada ya matokeo kutangazwa na kwa mujibu wa Kanuni za Mahakama ya Juu kama ambavyo ilitumika katika kesi ya Uchaguzi wa Rais mwaka 2017.

Jengo la Mahakama ya juu ya Kenya. Picha na The Standard.

Ayora alishauriwa kutafuta wakili wa kumsaidia kuendeleza hatua aliyokusudia ya kisheria, ambapo hata hivyo, iligongwa muhuri kama ilivyopokelewa na Ofisi ya Jaji Mkuu akisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilifaa kufanya uchaguzi huru na wa haki na kuomba maagizo ya marudio ya urais.

Barua hiyo yenye kurasa moja ilisomeka kuwa, “Ninaandika kueleza hali isiyoridhisha ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa wagombeaji urais ambayo yalitangazwa na mwenyekiti wa IEBC ,Wafula Chebukati Agosti 15, 2022.”

Kwa mujibu wa Ayora, anaamini kuwa matokeo ya uchaguzi wa urais si ya kuaminika kufuatia uamuzi wa makamishna wanne wa kuyakana na kusema, “Ni matumaini yangu Mahakama itazingatia ombi langu na kuhakikisha haki zangu za kidemokrasia zinatimizwa na ninaomba korti iahirishe kuapishwa kwa rais mteule.”

Usikilizwaji wa moja ya mashauri ndani ya Mahakama ya Juu nchini Kenya. Picha na Baz Ratner/Reuters.

Kulingana na sheria za 2017, kuwasilisha ombi la uchaguzi wa urais kunahitaji mlalamishi awe na kima cha chini cha Shilingi Milioni 1.5 ili kuzingatia madai, kugonga mhuri na Msajili shilingi milioni 1 kwa ajili ya gharama zitakazotumika wakati wa shauri, Shilingi 500,000 za kufungua jalada na Shilingi 20,000 pia hutozwa kwa mlalamikiwa anapowasilisha jibu la ombi.

Aidha, kutuma notisi ya hoja ni Shilingi 1,500, notisi ya hoja chini ya cheti cha dharura Shilingi 2,750 na kuwasilisha notisi ya nia ya kutopinga ombi ni Shilingi 4,000, huku kuwasilisha viambatisho ikiwa ni Shilingi 50 kwa kila karatasi na kuwasilisha mawasilisho yaliyoandikwa ikiwa ni Shilingi 50 kwa kila karatasi.

Ingawa maamuzi ya Ayora ni ya haki kisheria iliyothibitishwa na Katiba, lakini kwa gharama hizo huenda akashindwa au kufanikisha kulingana na uwezo alionao na hivyo suala lake bado limeacha mianya ya maswali kwamba huenda wapo watu nyuma yake waliomtanguliza mbele ama kinyume chake.

Kenya: Karua amtaka Ruto aache kuvunja sheria
Mashahidi wizi wa vifurushi wagoma kutokea hadharani