Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans van Pluijm, amesema amefanya maandalizi mazuri na kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Young Afrcans kuhakikisha wanapata matokeo chanya.
Young Africans itakuwa mgeni wa Singida Big Stars katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa baadae leo Alhamis (Mei 04) katika Uwanja wa CCM Liti, mjini Singida.
Kocha Hans amesema licha ya ligi kuwa ukingoni, wapo makini na michezo yote ilizosalia ili kufikia malengo yao na watahakikisha mchezo wa leo dhidi ya Young Africans wanavuna alama tatu muhimu.
“Tunatambua ubora wa kikosi cha Young Africans, kwa sababu wametoka kucheza Robo Fainali, nimewaona na ninaimani vijana wangu maelekezo watafuata niliyowapa na kupata matokeo katika mchezo huo,” amesema Pluijm.
Amesema licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, sio sababu ya kukubali kupoteza kwa mara ya pili, na kwamba wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanautumia vema uwanja wao wa nyumbani.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya pili msimu huu wa Ligi Kuu baada ya mchezo wa kwanza katika Dimba la Benjamin Mkapa, Singida Big Stars kukubali kipigo cha mabao 4-1.
Young Africans ambao ni mabingwa watetezi wanaongoza ligi hiyo wakiwa na alama 68 huku Singida Big Stars wakiwa nafasi ya tatu na alama 51.