Katika karne ya 15, mahitaji ya uchumi wa kimataifa yalisababisha kuongezeka kwa biashara ya watumwa hasa kutoka Afrika, ambapo mamilioni walikamatwa na watawala wa milki kwenye pwani za Afrika au Waarabu na kuuzwa kwa wafanyabiashara Wazungu waliowapeleka Amerika kufanya kazi kwenye mashamba makubwa ya miwa na pamba.
Biashara ya utumwa ilianza kupingwa zaidi tangu mwisho wa karne ya 18. Mkutano wa Vienna wa mwaka 1814-1815 ndiyo ulikuwa wa kwanza wa kimataifa uliolenga kukataza biashara ya watumwa kutoka Afrika.
Hata hivyo biashara hiyo haramu iliendelea kwa miaka kadhaa hasa upande wa bahari Hindi ambako wanafanyabiashara kama Tippu Tip waliendelea kukamata watumwa na kuwapeleka Pwani na Zanzibar kulikokuwa na soko la watumwa kubwa kuliko yote.
Ukoloni ulimaliza kwa kiasi kikubwa biashara hiyo Afrika pia, ingawa Mauritania ilifanya utumwa kuwa kosa la jinai mwaka 2007 tu.
Tangu karne ya 20 utumwa na pia biashara ya watumwa zimepigwa marufuku katika mapatano ya kimataifa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni imeibuka biashara mpya tena chafu zaidi, ingawa duniani hakuna utumwa tena kisheria, lakini hii ya wanawake na mabinti wanaouzwa kwa kazi haramu ya ukahaba kati ya nchi na nchi imeikumba dunia ya sasa. Jamii inapaswa kujihadhari na biashara hii, yenye chukizo kubwa kubwa sana kwa mwenyezi Mungu.