Wapare ni kabila kutoka milima ya Pare, Mkoa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa nchi ya Tanzania, lakini pia wapo katika wilaya ya Moshi sehemu za Chekereni, Himo, Mabungo, Uchira, Moshi mjini, pia katika wilaya ya Hai sehemu za Rundugai na mto Weruweru na katika wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, sehemu za Bumbuli na Mavumo.
Wapare kwa asili hujiita Vaasu ikiwa na maana ya “vareasa” au “watu wanaotumia pinde na mishale” ikiwemo ya sumu.
Wapare inasemekana wametoka katika nchi ya Kenya sehemu za Taita, Taveta na Ukamba pamoja na Wachaga. Wachaga walitangulia kuingia Tanzania (Tanganyika kwa muda huo) wakawahi kuishi maeneo yenye rutuba hasa kuzunguka mlima Kilimanjaro.
Wapare walikuja baadaye na walipotaka kuishi na Wachaga ndipo vita vikatokea kati ya Wapare na Wachaga. Ili kuepusha umwagaji damu zaidi Wapare walisogea kusini zaidi kuelekea mkoa wa Tanga.
Wana ukaribu na makabila ya Mkoa wa Tanga hasa Wasambaa, Wazigua na Wanguu. Ukaribu wao uko katika lugha ambapo maneno mengi ya makabila haya yanafanana.
Chakula kikuu kwa wapare kilikuwa ni makande (mchanganyiko wa mahindi na maharage). Aghalabu chakula hiki kiliandaliwa siku ya Ijumaa jioni hadi Jumapili jioni ili watu waweze kupumzika vizuri mwisho wa wiki bila kuwaza masuala ya upishi.
Wapere wengi pia wanapenda sana Samaki na ndiyo maana utawasikia watani wao wakuu yaani Wachaga wakiwatania kuwa Wapare wanakula ugali kwa picha ya samaki. Huu ni utani ulioasisiwa na wachagga baada ya kutembelea kaya nyingi za wapare na kukuta wamehifadhi samaki. Hapo ndipo mchagga mmoja alisikika akisema “Yesu yaani wapare wanapenda samaki, kila nyumba unayoingia utakutana na samaki. Yaani siku wakikosa samamki watakula ugali kwa picha ya samaki”. Utani huo ulikuzwa na wachagga hadi ukaonekana kama ni kweli, ukizingatia wachagga wametapakaa nchi nzima.
Hata hivyo wapare nao wana utani wao kwa wachagga unaosema “Muagha wedi ni ula efwie”. Yaani “mchaga mzuri ni yule aliyekufa” wakimaanisha kwamba wachagga wote ni walaghai na wadhulumishi wakati wote wa maisha yao. Ni mpaka atakapokufa ndipo ulaghai na udhulumishi wake vitaisha.
Wapare pia ni kabila la watu wanaopenda haki (yaani hawapendi kuonewa wala kumuonea mtu). Ndiyo maana watu wengine wanadhani wanapenda kesi, bali kesi ni njia mojawapo ya kuhakikisha haki inatendeka katika jamii. Utawasikia watu wengine wakidai kuwa Mpare yupo tayari kuuza ng’ombe kwa kesi ya kuku. Dhuluma kwa Wapare ni kitu kilichokuwa kimepigwa marufuku hata kwenye matambiko yao, japo siku hizi kuna uwezekano baadhi yao wakawa hawana sifa hii tena.