Wanyiramba (Wanilamba) ni kabila la Tanzania linalopatokana mpakani mwa mikoa ya Singida na Shinyanga. Lugha yao ni Kinyiramba.
Jina la kabila hilo lilitokana na njaa, kwani Hapo Kale Wanyiramba na Wanyisanzu walikuwa katika kundi mojawapo lililoelekea mashariki hadi maeneo ya Ziwa Nyanza (Victoria) hadi katika kisiwa cha Ukerewe kilichopo katika ziwa hilo kubwa zaidi barani Afrika.
Kundi hilo liliondoka katika kisiwa cha Ukerewe hadi Kisiwa cha Uzinza, na baadaye wakahama hadi maeneo ya Tabora ambako waligawanyiaka kundi moja likielekea kusini na inasemekana ndio waliokuja kuwa Wagogo na Wanyaturu huku kundi lingine likiendelea kuelekea Mashariki kupitia mlima Sekenke hadi Kisiriri.
Wanyiramba na Wanyisanzu waliishi Kisiriri kwa muda mrefu hadi ulipotokea ukame mkubwa sana uliosababisha njaa katika eneo hilo. Katika harakati za kukabiliana na tatizo la njaa, watu hao waliamua kula mboa za majani ya mlenda uliokaushwa zijulikanazo kama “ndalu” kama chakula chao kikuu.
Kutokana na kula “ndalu” kwa mtindo wa kulamba, watu wa makabila mengine ya kibantu walivyowaona wakawaita “wenye kulamba” na baadaye likabadilika hadi kuwa “wenyilamba” hadi “Wanyiramba”. Wanyisanzu na Wanyiramba walikuwa kabila moja wakati huo na wote walifahamika kama Wanyiramba baada ya njaa hiyo.
Baadaye Wanyisanzu/Waihanzu waliondoka hapo Kisiriri kuelekea pori la Mkalama wakiwa na mifugo yao na familia zao.
Walipofika katika pori hilo ili kujilinda na wanyama wakali wakajenga nyumba na kuzungushia maboma ya miba maarufu kama “masanzu/mahanzu”. Baadaye Wanyiramba walipowaona wenzao (Wanyisanzu/Waihanzu) wamezungushia nyumba zao kwa Maboma ya “masanzu/mahanzu” ndipo walipoanza kuwaita hawa ni wanyisanzu au waihanzu.
Hivyo ndivyo yalivyazaliwa majina ya Wanyiramba na Wanyisanzu wenye historia inayofanana na kwa mtu mgeni anaweza kudhani kuwa hakuna tofauti baina yao, lakini ukweli ni kuwa kuna tofauti kubwa sana baina yao.