Julai 7, 1954 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliongoza kikao cha Watanganyika 17 mjini (jijini) Dar es Salaam, kuanzisha chama cha kwanza cha siasa kilichoitwa “Tanganyika African National Union” (TANU).
Kikao hicho kilimchagua Mwalimu Nyerere kuwa Rais wa TANU. Alikuwa Rais pekee wa TANU mpaka mwaka 1977, TANU ilipoungana na ASP kuunda Chama Cha Mapinduzi au kwa kifupi CCM.
Lengo la kwanza la TANU lilikuwa kuleta Uhuru wa Tanganyika na kazi ya kwanza ya TANU ilikuwa kuwatayarisha Watanganyika kwa kujitawala wenyewe.
Harakati za kutafuta uhuru wa Tanganyika zilizoongozwa na Mwalimu Nyerere hazikuwa rahisi kwa sababu hiyo baada ya kupatikana uhuru, Nyerere aliitwa “Baba wa Taifa” ikiwa na maana ya mtu aliyeongoza juhudi za kutafuta uhuru na ujenzi wa Taifa jipya.
Nyerere alijua fika sababu kwa nini mababu zetu hawakufanikiwa kukomboa nchi yao, kwani alikuwa mwanahistoria na alijua kuwa hakuwa mtu wa kwanza kuongoza juhudi za kutafuta uhuru.
Wananchi wengi walitafuta uhuru kwa udi na uvumba enzi za Mjerumani, wakaishia kujiua au kunyongwa kwa kuthubutu kutafuta uhuru wa nchi yao.
Kutokana na hali hiyo, aligundua kuwa bila kuwa na umoja mkubwa uhuru usingepatikana.
Nyerere aligundua pia kwamba ilikuwa kazi bure kujaribu kumfukuza Mwingereza kwa kutumia silaha. Akaja na kaulimbiu ya “Umoja na Amani.”
Silaha ya umoja na amani zikatumika na zikafanikisha juhudi za kutafuta uhuru zilizoongozwa na Mwalimu Nyerere.
Aliendelea na juhudi za kutafuta uhuru bila kukata tamaa kwani alikuwa jasiri, angekuwa mtu wa kukata tamaa basi asingechelewa kuondokana na uongozi wa TANU.
Agosti 1954, mwezi mmoja tu tangu ilipozaliwa TANU, uliitishwa mkutano wa kwanza wa hadhara wa TANU Dar es Salaam eneo la Mnazi Mmoja.
Hapa unaweza kuona ni jinsi gani ilikatisha tamaa!, Mkutano huo ulihudhuriwa na watu sitini tu ingawa ulitangazwa maeneo yote ya Dar es Salaam, hali hiyo ilikuwa hivyo hivyo mikoani.
Mkutano wa kwanza wa TANU uliohutubiwa na Mwalimu Nyerere mjini Masasi mwaka 1955 ulihudhuriwa na watu kumi na mmoja tu.
Machi 21, 1955 Nyerere aliporudi shuleni Pugu akitokea Umoja wa Mataifa nchini Marekani, kesho yake alitakiwa achague kuacha ualimu au siasa.
Nyerere aliamua kuacha ualimu ili aendelee kuongoza harakati za kutafuta uhuru, huku akiwa hana hakika siasa ingemfikisha wapi.
Hivyo Nyerere akaacha kazi iliyokuwa ikimpatia riziki ili aendelee na juhudi zake za kutafuta uhuru. Huo haukuwa uzalendo wa kawaida.
1957 Nyerere alipigwa marufuku kuhutubia mikutano ya hadhara kwa miezi sita, wakati Serikali ya Mwingereza ilipodai kuwa hotuba zake zilikuwa zikichochea raia kuchukia Serikali ya Malkia.
1958 aliletwa mahakamani kwa madai kuwa alikuwa amewakashifu wakuu wawili wa wilaya wa kikoloni. Akahukumiwa kutoa faini shilingi elfu tatu au kifungo cha miezi sita.
Historia hii inathibitsha kamba Mwalimu Nyerere hakufanya kazi ya kawaida katika kutafuta uhuru.
Hakuwa pekee yake, alikuwa na mama Maria ambaye hakuhofia kuishi na mtu aliyekuwa akichukiwa na watawala.
Labda uhuru usingepatikana bila Nyerere, au bila Nyerere Tanganyika ingechelewa kupata uhuru au ingepata uhuru kwa kumwaga damu.