Dunia ina mambo, ndivyo unaweza kusema!! Katika hali isiyotarajiwa Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Nipashe Marco Maduhu amevunja simu yake ya mkononi ‘Smartphone’ baada ya mtandao katika simu hiyo kukatika na kuzimika mara kwa mara wakati akiendelea na semina mtandaoni kupitia mtandao wa Zoom.
Tukio hilo lililozua gumzo la aina yake limejiri katika ofisi ya klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club), Mjini Shinyanga.
Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa wakati Maduhu akiendelea na semina mtandaoni tangu saa tatu asubuhi, simu yake ilikuwa inazima na kukata mtandao mara kwa mara na kumfanya ashindwe kufuatilia kwa ufanisi zaidi mafunzo yaliyokuwa yanaendelea kwenye semina kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kupitia mtandao Zoom.
Wamesema kutokana na hali hiyo, ilipofika saa saba na dakika 40 Maduhu aliibamiza chini simu hiyo na kuipasua pasua kisha kutoka nje na kuitupa huku akisema haiwezekani kuendelea na simu inayoleta usumbufu wakati anafanya mambo ya maana.
Maduhu amesema amelazimika kuvunja simu hiyo kwa sababu ilikuwa inamkwamisha kuendelea na semina yake Zoom hivyo haoni sababu ya kuendelea na simu hiyo.
“Simu imeniletea ujinga ni bora kununua simu nyingine tu, haiwezekani nafanya mambo ya msingi halafu simu inaleta ujinga”, amesema Maduhu wakti akizungumza na chombo kimoja cha habari mkoani humo.
Vipi ndugu msomaji wa Dar24, simu yako ‘ikikuzingua’ unaweza kuivunjavunja ama utaivumilia tu?