Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umewashukuru Waandishi wa Habari na Vyombo vyao, kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa msimu wote wa 2021/22, ambao rasmi utafikia tamati Kesho Alhamis (Juni 29).
Young Africans tayari imeshatangaza na kukabidhiwa Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu, huku ikitarajia kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar Kesho katika mchezo wake wa mwisho.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Hassan Bumbuli amezungumza na Dar24 amesema, wanathamini na kutambua kazi kubwa iliyofanywa na Waandishi wa Habari kupitia vyombo vyao kuisemea mazuri klabu yao.
Amesema kwa muda wa msimu wote, idara yake imefanya kazi kwa weledi mkubwa kwa ushirikiano na Waandishi wa Habari, ambao walichagiza hamasa kwa Mashabiki na Wanachama wao kufika viwanjani kuishangilia timu yao.
“Tunawashukuru sana Waandishi wa Habari na Vyombo vyao, tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa hadi kufikia mafanikio ya kutwaa Ubingwa wa Tanzania bara msimu huu.”
“Wapo wachache ambao walitaka kuharibu, lakini kwa uungwana tunasema tumewasamehe, lakini kwa walio wengi tulisafiri katika safari yetu hii ya mafanikio, tunaamini msimu ujao tutaendeleza ushirikiano ambao unaendelea kukomaa baina yetu.”
“Hata nyinyi Dar24 mmefanya kazi kubwa sana, mara kadhaa tulikutana kwenye viwanja vya mikoani na mlifanya kazi yenu kwa weledi mkubwa sana, kwa hiyo na nyinyi mna mchango mkubwa sana kwa mafanikio haya tulioyapata Young Africans.”
Amesema Bumbuli Licha ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu, Young Africans pia inashikilia Rekodi ya kuwa klabu pekee ambayo haijapoteza mchezo wa ligi hiyo, ikisaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa kesho uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.