Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amerejea nchini na kupokelewa na wafuasi wa chama hicho, ndugu na marafiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro, KIA.
Lema, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Arusha mjini alianza safari yake ya kurejea nchini akitokea Canada na msafara wake unaelekea Arusha ambapo anarajiwa kufanya mkutano wa hadhara hii leo Machi 1, 2023.
Taarifa ya kurejea kwa Lema ambayo ilitolewa na CHADEMA January 31, 2023 ilisema Lema aliondoka nchini na kuelekea Kenya tarehe 8 November 2020 ambako alikaa kwa mwezi mmoja na baadaye December 8, 2020 alielekea nchini Canada ambako alipata hifadhi ya kisiasa, kutokana na uwepo kwa tishio la kuuawa yeye na Familia yake.
Mara baada ya kuwasili nchini, Lema pia anatarajia kuongoza kikao cha Kamati ya Utendaji ya Kanda na Baraza la Uongozi la Kanda ya Kaskazini, ziara za mikutano ya hadhara na vikao vya ndani kwenye Mikoa yote ya kanda ya Kaskazini ya Tanga, Kllimanjaro, Arusha na Manyara.