Mwili wa Mariam Kighendi (35) na Mwanaye Amanda Mutheu (4) tayari imeopolewa katika Feri ya Likoni, Mombasa huku ndugu na mume wa marehemu, John Wambua wakishuhudia baada ya gari lenye usajili wa namba KCB 289C kudumbukia na kuopolewa katika bahari ya hindi saa chache zilizopita.
Tayari miili hiyo imekimbizwa mochwari kwa ajili ya kusafishwa na kuandaliwa kwa mazishi.
Mume wa Marehemu, Wambura amehudhuria tukio hilo la uopoaji zoezi lililotumia takribani siku 13 tangu kudumbukia kwake.
Aidha, maafisa wa uchunguzi pia wamehudhuria tukio hilo la uokoaji na wapo tayari muda wowote kuanza uchunguzi wa tukio hilo.
Msemaji wa Serikali, Cyrus Oguan amesema iliwalazimu kukodisha vifaa vyenye teknolojia kubwa kusaidia kuopoa gari hilo lililokuwa na miili ya mama na mwanaye.
Mariam na mwanaye walifariki baada ya gari lao kuteleza kutoka kwenye kivuko kilipokuwa kinakaribia kutia nanga na kuzama baharini wakati wakivuka bahari kwa kutumia kivuko cha MV Harambee.
Tukio hilo lilitokea Septemba 29, mwaka huu katika feri ya Likoni nchini Kenya.