Hatua ya Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, kumfuta kazi waziri wa ulinzi na yule wa mambo ya ndani, imeibua mjadala kuhusu hatma ya utekelezaji wa mkataba wa amani uliotiwa saini na viongozi wa nchi hiyo.
Msemaji katika Ofisi ya rais Lily Martin Manyiel, amesema hakuna sababu, inayoweza kuelezwa kwa sasa kuhusu hatua ya kufutwa kazi kwa wawili hao, na maamuzi ya Mawaziri wapya, hayajafanyika.
Kwa mujibu wa mkataba wa amani wa mwaka 2018, ambao haujatejelezwa kikamilifu, nafasi ya Waziri wa Ulinzi inapaswa kutolewa kutoka upanda wa Machar.
Hata hivyo, Kiir amekiuka mkataba huo na kuamua kuwa Waziri ajaye wa Ulinzi atatoka kwenye chama chake huku ule wa usalama wa ndani atatoka upande wa Machar.
Msemaji wa Puok Both Baluang, amesema mabadiliko hayo yanakwenda kinyume na mkataba wa amani, unaoweza kusababisha changamoto katika serikali ya pamoja kati ya Kiir na Machar katika siku zijazo.
Mchambuzi Dr Brayan Wanyama amesema kuwafuta kazi kutayumbisha maelewano na utulivu ambao umekuwepo nchini humo.
“Hatua ya kuwafuta kazi itayumbisha pakubwa maelewano na vile vile utulivu ambao umekuwepo na mambo hayatakuwa sawa kama vile yalivyokuwa hapo awali.”ameeleza Dr Brayan Wanyama
Waliofutwa kazi ni pamoja na mke wa makamu wa kwanza wa rais, Riek Machar, Angelina Teny na Mahmoud Solomon.