Ufaransa imemtaka balozi wake nchini Uturuki kurejea nyumbani kwa mashauriano baada ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kusema kuwa rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron anahitaji matibabu ya afya ya akili na pia kutoa matamshi mengine ambayo serikali ya Ufaransa imeyataja kuwa ya ujeuri usiokubalika.
Rais Erdogan alitilia shaka hali ya akili ya Rais wa Ufaransa huku akikosoa mtazamo wake kuhusu uislamu na waislamu.
Matamshi ya Rais Erdogan aliyatoa wakati wa mkutano wa chama kimoja nchini humo yalikuwa yakijibu matamshi yaliotolewa na Macron mwezi huu kuhusu matatizo yanayosababishwa na waislamu wa itikadi kali nchini Ufaransa wanaojihusisha na kile kiongozi huyo wa Ufaransa alichokitaja kuwa ”kujitenga kwa waislamu.”
Wakati huo huo, takriban watu 200 walifanya maandamano nje ya makazi ya balozi wa Ufaransa nchini Israeli dhidi ya rais Macron baada ya kuapa kuwa nchi yake haitaondoa vinyago vinavyomfananisha mtume Mohammed.
Maandamano hayo yaliandaliwa katika eneo la Jaffa mjini Tel Aviv, baada ya sala za Jioni.