Uongozi wa Young Africans umeendelea kusisitiza suala la kutomuweka Sokoni Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele, ambaye anatajwa kuwania na klabu kadhaa Barani Afrika.
Mshambuliaji huyo ambaye amemaliza kinara wa kupachika mabao kwenye kikosi cha Young Africans msimu wa 2021/22, juma lililopita alihusishwa na mpango wa kuwindwa na Klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Mgombea Urais wa klabu hiyo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Usajili Hersi Said, ametilia mkazo wa kutowekwa sokoni kwa Mshambuliaji huyo, alipohojiwa na Wasafi FM mapema leo Jumatano (Julai 07) jijini Dar es salaam.
Hersi amesema Klabu kadhaa na Mawakala wamekua wakipishana kuulizia uwezekano wa kuuzwa kwa Mshambuliaji, na wengine wanampigia simu yeye binafsi kuulizia dili hilo.
“Nikikuonyesha simu yangu hapa, kuna Request nyingi za ma-agents wakitaka huduma ya Fiston Mayele, but ‘He Is Not For Sale’.”
“Young Africans Level tuliofikia ni kuchukua wachezaji kutoka kwao (Kaize Chiefs), hata yule Nahodha wao sisi tunamuhitaji, sio wao kuchukua kwetu.” Amesema Hersi
Fiston Mayele amemaliza msimu wake wa Kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara akifunga mabao 16, akitanguliwa na Mshambuliaji mzawa wa Klabu ya Geita Gold FC, George Mpole aliyepachika mabao 17.
Mayele alisajiliwa Young Africans mwanzoni mwa msimu wa 2022/21 akitokea nchini kwao DR Congo alipokua akiitumikia klabu ya AS Vita ya mjini Kinshasa.