Chama cha Soka nchini Sierra Leone (SLFA), kimeanza kufanya uchunguzi wa matokeo ya michezo miwili iliyomalizika kwa matokeo ya kustaajabisha mwishoni mwa juma lililopita.

Michezo hiyo miwili ilimalizika kwa timu kufungana jumla ya maboa 187, ambayo yalizua taharuki kwa wadau wa soka Barani Afrika na nje ya Bara hilo.

Michezo hiyo iliunguruma Jumapili (Julai 03), ambapo timu ya Kahunla Rangers ilisambaratisha Lumbebu United mabao 95-0 huku Kono’s Gulf FC ikiizaba Koquima Lebanon mabao 91-1.

Timu zote mbili zilikuwa kwenye kinyang’anyiro cha kupanda daraja zikiwa na alama sawa, lakini uamuzi wa nani atakayepanda daraja ulikuwa ukisubiri ama kufungwa kwa timu mojawapo, na kama zingeshinda zote basi ingeamuliwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Hadi timu zote mbili shindani zinakwenda mapumziko matokeo kwa Kahunla Rangers iliongoza kwa goli 2-0 na Kono’s Gulf FC ikiwa na mabao 7-1.

Mara baada ya matokeo ya mwisho Rais wa Chama cha Soka nchini humo, Thomas Daddy Brima ameagiza kuanza kufanywa kwa uchunguzi huku akisema, “Hatuwezi kuacha tabia ya kama hiyo bila kutoa adhabu na wale waliohusika watalazimika kufika mbele ya tume ya kupambana na rushwa na watatendewa sawa na atendo yao”.

Mapema mwezi Juni nchini Afrika Kusini kulitokea changamoto kama hiyo ya upangaji wa matokeo, ambapo timu za daraja la nne ziliruhusu makumi ya mabao, hali iliyofanya Viongozi wa vilabu husika kusimamishwa kujihusisha na soka kwa miaka 6 hadi 8.

Mwaka 2013, nchini Nigeria pia kulitokea sintofahamu kwa Klabu ya soka ya Plateau United kuitandika Akurba FC mabao 79-0, wakati Police Machine FC yenyewe ikishinda kwa jumla ya magoli 67-0 dhidi ya Babayaro FC.

Hersi Said: Fiston Mayele hauzwi NG'O
Wananchi hali mbaya, msaada wa haraka wahitajika