Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limethibitisha tarehe ya kuanza kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa Wanawake 2022.

Ofisa Mtendaji wa CECAFA, Auka Gecheo amesema michuano hiyo ambayo pia itakuwa ya mchujo wa kuwania kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ya Wanawake 2022, itafanyika Julai 28 hadi Agosti 10 jijini Arusha, Tanzania.

 “Tutakuwa na timu nane ambazo zimethibitisha kushiriki katika mashindano na timu nne zimewekwa katika kila kundi.  Viwanja vya Arusha Abeid na Black Rhino Acadamy, Karatu ndio vitatumika katika michuano hiyo,” ameongeza Gecheo.

Timu nane zitakazoshiriki ni She Corporate FC (Uganda), Simba Queens (Tanzania), Yei Joint Stars FC (Sudan Kusini), Warrior Queens (Zanzibar), Fofila PF (Burundi), AS Kigali Women’s FC (Rwanda), GRFC (Djibouti) na Commercial Bank of  Ethiopia (Ethiopia)

Mabingwa watetezi Vihiga Queens FC kutoka Kenya hawatashiriki michuano hiyo, kufuatia nchi ya Kenya kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha Shirikisho la soka Duniani ‘FIFA’.

Jumapili (Julai 03), Shirikisho la Soka Barani Afrika0 ‘CAF’ ilitangaza kuwa Morocco itakuwa mwenyeji wa Ligi ya Mabingwa ya Wanawake kwa mwaka huu 2022.

Timu ya wanawake ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo, baada ya kuibuka Mabingwa kwenye Fainali za kwanza zilizopigwa jijini Cairo, Misri.

Wananchi hali mbaya, msaada wa haraka wahitajika
Maliasili na Utalii 'watisha' matumizi ya fedha za umma