Uongozi wa Young Africans umethibitisha kupokea ofa kutoka kwenye klabu kadhaa za Barani Afrika zikimlenga mshambuliaji wao kutoka Burkina Fasso Yocouba Sogne.
Young Africans wamefunguka ukweli wa jambo hilo, kufuatia Mshambuliaji huyo kuendelea kuwa gumzo miongoni mwa wachezaji wa klabu hiyo kwa msimu huu 2020/21, ambao utafikia ukingoni baadae mwezi huu.
Siri ya kuwaniwa kwa mshambuliaji huyo imefichuliwa na Makamu Mwenyekiti Kamati ya Usajili Young Africans Injinia Hersi Said, ambapo amesema baada ya ofa hizo kupokelewa wanaendelea kuzifanyia kazi, hivyo kama wataona kuna umuhimu wa kumuuza watafanya hivyo mwishoni mwa msimu huu.
Amesema kuwaniwa kwa Mshambuliaji huyo kunadhihirisha walifanya usajili sahihi mwanzoni mwa msimu huu, hivyo amewahimiza Wanachama na Mashabiki wa Young Africans kuendelea kupuuza kauli iliyowahi kutoka na kudai klabu hiyo imeokota okota wachezaji.
“Tuna ofa nyingi zinazomhitaji mshambuliaji wetu Yacouba Songne ambazo klabu bado inaendelea kuzifuatilia kwa kuzifanyia kazi, hii kwetu ni ishara kwamba hatukuokota wachezaji, tulitulia na kusaka watu sahihi kwa klabu yetu” amesema injinia Hersi
Yacouba Sogne amekua mchezaji pekee ndani ya kikosi cha Young Africans aliefunga mabao mengi kuliko yoyote klabuni hapo.