Mshambuliaji kutoka Korea Kusini Heung-Min Son, anahisi uvumi unaoendelea kuhusu Harry Kane sio rahisi kwa mchezaji mwenzake huyo, lakini amesifu weledi wa nahodha wa klabu hiyo.

Son na Kane wametua Singapore kwa awamu ya mwisho ya ziara yao ya awali ya kujiandaa na msimu mpya baada ya siku chache zenye matukio mengi mjini Bangkok nchini Thailand.

Hali ya hewa ilisababisha mechi ya kirafiki kati ya Tottenham na Leicester kufutiliwa mbali Jumapili na siku moja mapema mwandishi wa habari kutoka Jarida la Ujerumani, Bild, alizindua jezi ya Bayern Munich yenye ‘Kane 9 mgongoni kwa kocha mkuu mpya wa Spurs, Ange Postecoglou katika mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya mechi.

Postecoglou hakufurahishwa sana, lakini kelele za Kane hazioneshi dalili ya kuondoka, huku Bayern ikitarajiwa kurejea na ofa ya tatu baadaye mwezi huu.

Kane, ambaye anatekeleza majukumu ya unahodha wakati wa ziara ya Tottenham baada ya Hugo Lloris kuachwa England ili kukamilisha uhamisho wa kuihama klabu hiyo, amepongezwa na mshirika wake wa muda mrefu.

“Harry amekuwa mzuri kwangu.” alisema Son akiwaambia waandishi wa habari huko Bangkok. “Yeye ni mtaalamu, daima anafanya kazi kwa bidii.

“Hajawahi kuonesha mawazo yoyote juu yake mwenyewe. Kuna habari nyingi sana pia si rahisi kwake, lakini ni nahodha kwa sasa na anafanya kazi na timu.

“Haoneshi usumbufu wowote. Anapenda kuwa hapa. Ninampenda kama mchezaji. Ninamheshimu kikamilifu.

“Yeye ni mmoja wa washambuliaji bora zaidi duniani, amekuwa kwa miaka mitano, sita, saba mfululizo. Uamuzi utakuwa kati ya klabu na Harry na tunapaswa kuuheshimu.

“Siwezi kusema chochote kuhusu uamuzi wa mwisho kwa sababu sijui chochote. Labda Harry hajui. Inabidi tuşubiri tu.”

Kane ameingia miezi 12 ya mwisho ya mkataba wake pale Tottenham na Bayern wameongeza juhudi zao za kumsajili fowadi huyo mwezi huu, huku rais wao wa heshima Uli Hoeness akidai wiki iliyopita kuwa makubaliano binafsi yalikubaliwa kati ya klabu hiyo ya Ujerumani na nahodha huyo wa England.

Bayern wanaripotiwa kutuma maombi mawili ambayo hayakufanikiwa kwa Kane hadi sasa msimu huu wa majira ya joto, lakini Spurs bado wamedhamiria kumshikilia mfungaji wao huyo bora wa muda wote.

Mkataba mpya umetolewa kwa Kane na Tottenham, ambalo ni ongezeko kubwa katika mkataba wake wa sasa wa Pauni 200,000 kwa wiki, lakini hajafanya uamuzi wowote kuhusu mkataba huo mpya huku uvumi juu ya mustakabali wake ukiendelea.

Spurs wanatarajiwa kucheza na timu ya ndani ya Lion City Sailors huko Singapore kesho Jumatano (Julai 26) kabla ya kurejea England.

Shindano la kulala somo kwa wasiopumzisha mwili
Wanasiasa msipinge kila jambo la Serikali - Dkt. Kimei