Kampuni ya MICO International Halal Bureau of Certification (MIHB), imefanikiwa kupata cheti cha kimataifa kitakachoiwezesha kutoa ithibati ya Halal ya kimataifa kwa bidhaa mbalimbali ikiwemo nyama inayotumika nchini na inayosafirishwa kuuzwa nje ya nchi.
Kwa kupata cheti hicho kwa mara ya kwanza sasa Tanzania imepata kampuni iliyokidhi vigezo vya kimataifa vya ithibati ya Halal (MIHB) ambaye ni wakala wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Hafla ya kukabidhi cheti hicho imefanyika Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mwakilishi wa Mufti wa Tanzania ambaye ni Katibu wake, Musa Bin Hemed na wawakilishi wa taasisi ya Uturuki iliyotoa cheti hicho ya Hafsa Halal Murat Bayka na Jalal Sahal.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Sheikh Mwenda Said ambaye ni Mweka Hazina Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA), amesema cheti hicho kimetolewa baada ya BAKWATA kupitia mdau wake MICO International Halal Bureau Limited kuendesha mafunzo ya kuwaongezea wataalamu wao uwezo.
Amesema Hafsa Halal Certification and Food Import and Export Limited ya Uturuki kwa kushirikiana na MICO walianza kuwaongezea ujuzi watu hao kwa njia ya zoom kuanzia mwezi wa tatu mwaka huu na kuja kukamilisha mafunzo hayo ya ana kwa ana kuanzia Julai Mosi hadi sasa ambapo wamefikia viwango vinavyotakiwa kimataifa.
Akizungumzia umuhimu wa kuwa na cheti cha kimtaifa cha Halal, Sheikh Mwenda alisema bidhaa za Tanzania zitakubalika katika soko la kimataifa hasa nyama na kuongeza pato la taifa litakalosaidia kukuza uchumi na kuongeza wigo wa ajira lakini pia kupata na fedha za kigeni .
“Nchi ilikuwa inapata hasara kwasababu makampuni ya ndani yalikuwa yanachukua ithibati ya Halal nje ya nchi kama Australia, Quatar na kwingineko lakini sasa MICO Halal Tanzania itafanyakazi hiyo na hela zitabaki hapa nchini,” Amesema Sheikh Mwenda
Halikadhalika wameiomba serikali kupigia chapuo suala la ithibati katika nchi yetu kwa kuwataarifu wafanyabiashara, ambapo ithibati ya Halal nje ya nchi kama Afrika Kusini, Australia na kwingineko kuwa BAKWATA kupitia wakala wake MICO sasa wanatoa hiyo ithibati hapahapa nchini.