Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), umepangwa kufanyika Mei 12 ukitanguliwa na mkutano mkuu utakaoanza majira ya saa moja asubuhi.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Charles Rwechungura inaeleza kuwa uchaguzi huo utatanguliwa na ule wa mikoa utakaofanyika kati ya Aprili 14 au 15 ambapo nafasi zinazogombewa kwenye mikoa ni Mwenyekiti wa Mawakili wa Mkoa, Makamu Mwenyekiti, Mhasibu na Mwakilishi wa Mawakili waMkoa kwenye Mkutano mkuu.
Wengine ni mwenyekiti wa mkoa wa kamati ya msaada wa kisheria, mwenyekiti wa mkoa wa kamati ya elimu endelevu ya sheria, mwenyekiti wa mkoa wa kamati ya ustawi ya wanachama na mwakilishi wa mkoa kwenye kamati ya utendaji (EXCOM).
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Mei 10, wanachama wa mawakili vijana, watapiga kura kumchagua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu mkuu wa Chama cha Mawakili Vijana (AYL) wakati chaguzi za kanda zikifanyika siku moja baadaye.
Nafasi zitakazowaniwa kwenye kanda ni ya kiongozi wa kanda (council member), wawakilishi wawili wa mawakili wa kanda kwenye mkutano mkuu, mwakilishi wa kanda kwenye kamati ya utendaji (zonal EXCOM) na mwakilishi wa kanda wa mawakili vijana kwenye kamati ya utendaji (Zonal EXCOM).
Wengine kwa mujibu wa taarifa ya mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi iliyochapishwa kwenye gazeti l Mwananchi la leo Februari 2 ni mwakilishi wa kanda anayewakilisha mawakili wanawake kwenye kamati ya utendaji (Zonal EXCOM) na mwakilishi wa kanda anayewakilisha wenye ulemavu kwenye kamati ya utendaji (Zonal EXCOM).
Mei 12, wanachama wa TLS watapiga kura kuchagua rais mpya atakayechukua mikoba ya professa Edward Hoseah anayemaliza muhula wake wa pili na wa mwisho kugombea kwa mujibu wa sheria inayotoa kipindi kimoja cha kiongozi aliyepo madarakani kutetea kiti chake.
Dkt. Hoseah aliiongoza TLS tangu 2021 na kutetea kiti chake 2022. Nafasi nyingine zitazogombewa kwenye uchaguzi huo ni ya makamu wa rais na mweka hazina, huku kamati ikitarajiwa kutangaza mchakato wa kuanza kampeni wakati wowote.
Marais wengine waliowahi kuongoza TLS kwa miaka ya karibuni ni Tundu Lissu aliyekabidhi kijiti kwa Fatma Karume mwaka 2018, kisha Dk Rugemeleza Nshala (2019-2020), na Dk Hoseah 2021 hadi sasa.