Kampuni ya Kichina imepanga kujenga hoteli kubwa ya kifahari yenye vyumba 300 vya kulala, endapo itafikia makubaliano ya kiuwekezaji na Serikali.

Hoteli hiyo inatarajiwa kujengwa katika Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha na itakuwa hoteli kubwa zaidi nchini kwa idadi ya vyumba; na moja kati ya hoteli kubwa zaidi katika eneo la Kusini mwa Afrika, Mashariki na Kati.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali iko kwenye mazungumzo na muwekezaji huyo wa kichina na wanatarajia yatazaa matunda.

“Wawekezaji wa Kichina wako tayari kutekeleza mradi mapema kuanzia Oktoba mwaka huu kama mambo yataenda vizuri kama yalivyopangwa,” alisema Profesa Mkenda na kuongeza, “hii itakuwa hoteli kubwa zaidi Tanzania kwa idadi ya vyumba.”

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, wawekezaji hao wameshatembelea eneo la ardhi ambayo wanataka kuwekeza na wameridhishwa nalo.

Alisema Taasisi za Serikali ikiwa ni pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wakala wa kulinda mazingira pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii wako kwenye mazungumzo kuhusu uwekezaji huo.

Katibu Mkuu  huyo wa Wizara alieleza kuwa sababu za wawekezaji hao kuichagua Tanzania ni kutokana na juhudi za Serikali katika kuwavutia watalii wengi zaidi nchini.

Tanzania inategemea kupokea watalii 10,000 mwaka huu chini ya mpango unaosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania na Kampuni ya TouchRoad Intenational Holding.

Tayari kundi la wageni 300 lilishawasili nchini na kupokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

NB: Picha sio halisi

JPM atuma ujumbe kwa nchi za SADC kuhusu utegemezi
Walimu wamuangukia Rais Magufuli