Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amezitaka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini SADC kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyokuwa na umuhimu wowote.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya nne ya wiki ya viwanda, ambapo amesema kuwa kama vikwazo hivyo vikiondolewa basi maendeleo yatapiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Amesema kuwa nchi wanachama wa SADC ni lazima zishikane mikono ili kuweza kuleta maendeleo katika nchi husika na jumuiya kwa ujumla.

Aidha, Rais Magufuli amezitaka nchi hizo kufanyabiashara kwa pamoja ili ziweze kuondokana na kuwa tegemezi kutoka mataifa tajiri duniani kwani zinaweza kujitegemea kwakuwa zina malighafi za kutosha.

”Niziombe nchi wanachama wa SADC, ziondoe vikwazo hivi ambavyo vimekuwa ni tatizo kubwa na kero kwenye ufanyaji biashara, maana mpaka sasa bado nchi hizi zinasafirisha malighafi nje wakati tunaweza kuuziana ndani ya jumuiya na tukainua uchumi wetu,”amesema Rais Magufuli

Pia, Rais Magufuli amezishauri sekta binafsi kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kurahisisha ufanyaji biashara kwakuwa kutakuwa na faida kubwa kwa pande zote mbili yaani kati ya nchi na nchi ndani ya jumuiya ya SADC.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Innocent Bashungwa amesema kuwa wizara yake imejipanga kuhakikisha kunakuwepo na ushikiano wa kutosha na wenye tija ndani ya Jumuiya hiyo.

Naye, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amempongeza Rais Magufuli kwa kuweza kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, ambayo itapanua wigo wa kibiashara.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa SADC wenye kauli mbiu, “Mazingira Wezeshi ya Kibiashara kwa Maendeleo ya Jumuishi na Endelevu ya Viwanda.”

Wakuu wa nchi 16 wanachama wa SADC watakutana jijini Dar es Salaam Agosti 17 na 18 mwaka huu kujadili kiundani kauli mbiu hiyo.

SADC: Bashungwa awaonesha ‘fursa’ wadau wa sekta binafsi
Hoteli ya kifahari yenye vyumba 300 kujengwa nchini