Mvutano wa uhalali wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (Chakamwata) umesababisha chama hicho kumpigia goti Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.

Mratibu wa chama hicho, Emmanuel Patrick aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri amewazuia kufanya mkutano wao wa kuwachagua wajumbe wa Bodi ya Udhamini kwa madai kuwa hawakuwa na Bodi hiyo, hivyo kukosa uhalali kisheria.

Patrick alidai kuwa uamuzi huo ni sawa na kupigwa vita ili kisiendelee kwani waliitisha mkutano mkuu kwa dharura wakiwa na lengo la kupata Bodi ambayo Msajili amedai hawana.

Mratibu huyo amemuomba Rais Magufuli kuingilia kati na kuwaruhusu kuonana naye kwani wao wana lengo la kuwasaidia walimu na kwamba kitendo kilichofanywa na Msajili ni sawa na kukwamisha juhudi za Rais za kuwainua walimu.

“Tunamuomba mwalimu mwenzetu, Rais Magufuli aturuhusu tukutane naye, tumweleze namna watu ambao wana dhamana ya kusimamia walimu wanavyotaka kukwamisha juhudi zake, kwa sababu kumekuwa na mipango ya makusudi ya kutaka kukiua chama hiki chenye malengo ya kukomboa walimu wa nchi hii kwa maslahi ya Taifa,” Patrick anakaririwa.

Aidha, Patrick alieleza kuwa anaamini chama hicho kinapigwa vita kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya walimu wanaokihama Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) na kujiunga na chama hicho.

Mwenyekiti wa chama hicho, Japhet Joseph alieleza kuwa chama hicho kimesajiliwa na kina wanachama 12,000 nchini kote na kwamba chama hicho kinatoa maslahi zaidi kwa walimu kulinganisha na CWT, hivyo kuwavutia walimu wengi.

Msajili alikiandikia barua chama hicho akieleza kuwa kimekosa uhalali wa kuwa chama cha wafanyakazi kwakuwa hakina Bodi ya Udhamini ya kukisimamia.

Hoteli ya kifahari yenye vyumba 300 kujengwa nchini
LIVE: Rais Magufuli katika ufunguzi wa maonyesho ya wiki ya nne ya Viwanda SADC