Kiungo wa klabu ya Mtibwa Sugar Abdulhalim Humoud amewataka wachezaji wa Tanzania kutambua thamani ya kuitwa na kucheza kwenye kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars).
Humoud ambaye alitamba kwenye kikosi cha Taifa Stars wakati wa utawala wa kocha kutoka nchini Brazil Marcio Maximo, amesema baadhi ya wachezaji wamekua hawajui thamani ya kuitwa na kucheza kwenye timu hiyo, na badala yake huonyesha utovu wa nidhamu sambamba na kushindwa kujituma wanapopata nafasi ya kucheza.
Amesema Taifa Stars ina hadhi kubwa kwa kila mchezaji wa Tanzania, na kwa yoyote atakaepata nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo, hana budi kuonyesha heshima na uzalendo kwa maslahi ya watanzania wote.
“Napenda kuona kila mmoja anaeitwa kwenye timu ya taifa, basi aweze kuona ile thamani yake na timu ya taifa, kwa sababu timu ya taifa ni kitu kingine kabisa. Sisi tumecheza timu ya taifa kwa kipindi cha zamani, lakini mpka kesho tunatamani kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa sababu mchezaji anaecheza timu ya taifa, kiukweli kabisa ana heshima yake, huo ndio uhalisia na mambo yalivyo.”
“Ukishafikia hatua ya kukabidhiwa bendera ya nchi kupitia jezi uliovaa, inamaanisha unawawakilisha watu zaidi ya milioni 50, hivyo unapaswa kuonyesha thamani kwa niaba ya wale unaowawakilisha.” Alisema Humoud.
Akitolea mfano wa thamni ya timu ya taifa kwa wachezaji wa mataifa mengine, kiungo huyo mkongwe amesema baadhi yao wamekua wakikosa nafasi ya kuitwa kwenye timu zao za taifa, na kufikia hatua ya kuchukua maamuzi magumu ya kubadilisha uraia ili wacheze timu za taifa.
“Tuna mifano mingi duniani, baadhi ya wachezaji wameshabadilisha uraia kutokana na asili ya wazazi wao, ili atimize jukumu la kucheza kwenye timu ya taifa, sasa kwa hapa nyubani kila mmmoja anatakiwa kuitumia fursa hiyo kwa kujituma na kuwafurahisha watanzania wanaotaka kuona taifa Stars ikipiga hatua kubwa kimataifa.”
Wakati wa utawala wa kocha Maximo, Humoud aliitwa mara kwa mara kwenye kikosicha Taifa Stars, kutokana na kiwango kizuri alichokua nacho kwa wakati huo, na alipata nafasi ya kucheza kwenye michezo miwiwli ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Brazil na Ivory Coast mwaka 2010.
Siku za karibuni humoud amekua na wakati mgumu wa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kwa ajili ya kulitumikia taifa la Tanzania kimataifa.
Hata hivyo kwa msimu huu wa 2019/20 amekua na kiwango kizuri akiwa na klabu yake ya Mtibwa Sugar, hali ambayo imechangia kuhusishwa na mipango ya kutaka kusajiliwa na Young Africans.
Swali ni je? Kiwango alichokionyesha kiungo huyo kinaweza kumshawishi kocha mkuu wa Taifa Stars Ettiene Ndayiragije, kumrudisha kundini?