Bodi ya ligi Tanzania bara (TPLB) imetangaza msimamo wa kuendelea ama kuvunjwa kwa Ligi Kuu ya Soka Tanzania bara na ligi nyingine msimu huu wa 2019/20, katika kipindi hiki ambacho bado shughuli za kimichezo zimsimama.

Ligi kuu ya soka Tanzania bara na ligi nyingine za soka zimesimama kupisha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, hali ambayo inazua taharuki kwa wadau wa soka, ambao bado hawafahamu mustakabali wa kurudi ama kutokurudi kwa ligi hizo siku za karibuni.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Alsmas Kasongo amesema kwa sasa ni mapema mno kufikiria kumaliza msimu kutokana na janga la virusi vya Corona, lakini pia maamuzi yoyote yatatolewa na kamati ya Utendaji ya Shirikisho la soka nchini TFF.

Kasongo, amesema hakuna kanuni yoyote inayoelekeza hatua za kuchukuliwa pale ligi inaposhindikana kufika mwisho hivyo uamuzi wowote utaamuliwa na kikao cha Kamati ya Utendaji kwa kuwashirikisha wadau.

Aidha Kasongo amesema ni wasaa mzuri kwa TFF na wadau wake kukaa chini kutengeneza kanuni ambayo itaepusha sintofahamu juu ya hatua za kuchukuliwa pale ligi inapokwama.

“Kanuni hazisemi linapotokea janga kama hili nini kifanyike, zinazungumzia tu mchezo. Pengine ni wakati mwafaka kufanya maboresho ya kanuni baada ya janga hili,” amesema

Habarileo
Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB) Almas Kasongo.

Hata hivyo Rais wa TFF Wallace Karia amesema kwa sasa hakuna hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa hadi hapo Serikali itakapotaoa mwongozo wake.

Hivi karibuni kumeibuka mjadala baada ya baadhi ya wadau kupendekeza ligi imalizwe na vinara wa msimamo wa ligi kuu msimu huu Simba SC kutangazwa kuwa bingwa.

Mwanzoni mwa juma hili mkuu wa idara ya habari na mawasilino wa Young Africans Hassan Bumbuli alisema msimamo wa klabu hiyo ni kuona michezo iliyobaki inachezwa pale changamoto ya virusi Corona itakapomalizika, ili bingwa apatikane uwanjani.

Bumbuli alisema kimahesabu, Young Africans inaweza kufikisha alama 84 kama itashinda michezo yake iliyosalia hivyo wanaweza kushinda ubingwa kama ikitokea timu nyingine hazitafikisha idadi hiyo ya alama

Wakati huo huo kumekuwa na makundi tofauti miongoni mwa wadau wanaopendekeza nini kifanyike kama ikitokea ligi haitawezekana kumalizika.

Kundi la kwanza ni wale wanaotaka timu inayoongoza ligi ipewe ubingwa kisha kuwe na michezo michache za ‘play-off’ kusaka nafasi ya pili na timu za kushuka daraja.

Kundi jingine linataka subira iendelee kutawala ili mambo yatakapotulia basi ligi iweze kuendelea. Hata hivyo changamoto ni muda uliopo, kwani inawezekana jambo hilo likachukua muda mrefu pengine hata kuathiri muda wa kuanza msimu ujao.

Lakini pia wapo wanaopendekeza michezo ya playoff ichezwe kutafuta bingwa wa ligi kuu na timu zinazopaswa kushuka daraja huku kundi jingine likipendekeza msimu mzima ufutwe kama ilivyofanya nchi ya Uholanzi na Ufaransa.

Corona Tanzania: wagonjwa wapya 196, visa vyafikia 480
Saba wakamatwa wilayani Hai kukiuka bei elekezi ya Sukari