Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Ettiene Ndayiragije ameingilia kati hoja ya kupunguzwa kwa wachezaji wa kigeni kwenye klabu za ligi kuu ya soka Tanzania bara, iliyoibuliwa na Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa Na Michezo Harrison Mwakyembe.

Juzi na jana hoja hiyo ilikuwa na mashiko makubwa kufuatia kauli na makala iliyotolewa na mkuu wa Idara Ya Habari Na Mawasilino Wa Klabu Ya Simba Haji Sunday Ramadhan Manara, ambaye alipinga kata kata hoja hiyo kupewa nafasi, kwa kusisitiza itarudisha nyuma soka la Tanzania kwa kiasi kikubwa.

Kocha Ndayiragije amesema anaamini uwepo wa wachezaji wa kigeni kwa idadi yao kwa sasa kwenye kila klabu inatosha kutoa ushawishi kwa wachezaji wazawa kujituma na kuwania nafasi kwenye vikosi vya kwanza, hivyo kwake anajihisi faraja kwa kuamini hatua hiyo inaendelea kumpa kikosi bora kwa ajili ya michuano ya kimataifa.

“Kwa upande wangu hakuna tatizo, kwa sababu mpira ni kushindana, kwa hiyo tukiwa na wachezaji wakigeni wanaotoa ushindani kwa wachezaji wazawa inawawezesha kuwa na umakini wa kuhakikisha wanapambana kikamilifu, ili kuingia kwenye vikosi vya kwanza vya klabu zao,”

“Nina mifano mizuri kwa baadhi ya wachezaji wazawa ambao wameshapambana na kufanikiwa kuwaweka benchi wachezaji wakigeni, binafsi sina wasiwasi na hilo, kwa sababu ninaamini Tanzania ina wachezaji wenye uwezo mkubwa sana, hivyo changamoto ya uwepo wa wachezaji wengi wa wakigeni inawakumbusha majukumu yao, na mwishowe niwaite kwenye kikosi cha Taifa Stars.” Amesema Ndayiragije.

“Tukisema tuwapunguze wachezaji wakigeni, tutakoa muelekeo wa huko tuendapo, mimi ninashauri inapaswa kuachwa kama ilivyo kwa sasa, ili kutoa nafasi ya kila mmoja kujitambua, hasa katika uwajibikaji wa kuwania nafasi.”

Kocha Ndayiragije alitangazwa kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars, baada ya kukaimu nafasi hiyo kwa muda, kufuatia kutimuliwa kwa kocha kutoka Nigeria Emmanuel Amunike, ambaye alifanikisha ndoto za watanzania kuiona timu yao ikishiriki fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2019.

Kabla ya kuwa kocha wa Taifa Stars, Ndayiragije alivinoa vikosi vya klabu za Mbao FC ya Mwanza, Kinondoni Municipal Council (KMC FC) na Azam FC zote za jijini Dar es salaam.

Humoud: Wachezaji watambue thamani ya Taifa Stars
Tanzia: Mbunge Ndasa afariki dunia, Ndugai ahairisha vikao vya Bunge