Mbunge wa Jimbo la Sumve wilayani Kwimba mkoani Mwanza, (CCM) Richard Mganga Ndasa amefariki dunia mapema leo mkoani Dodoma.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, ameahirisha vikao vya bunge leo April 29,2020 baada ya kutokea kwa msiba wa mbunge huyo.

Ndugai amesema “kwa masikitiko makubwa bunge limepatwa na msiba mwingine mkubwa wa Richard Ndassa ambaye amefariki usiku wa kuamkia leo Aprili 29, 2020 mkoani Dodoma”.

“Waheshimiwa wabunge kufuatia msiba huo tulioupata taratibu mbalimbali za mazishi zimeanza kufanyika kwa mawasiliano kati ya ofisi yetu ya bunge pamoja na familia ya marehemu na upande wa serikali,” amesema Ndugai

Ndasa ametumikia jimbo la Sumve kwa vipindi vitano mfululizo na ni miongoni mwa waheshimiwa wabunge waandamizi walioingia bungeni toka mwaka 1995.

Marehemu alizaliwa Machi 21, 1959, na amefariki Aprili 29,2020 akiwa na miaka 64.

Katika utumishi wake wa Bunge la Tanzania amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali kama vile Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kamati ya Hesabu za Serikali, Kamati ya Maadili, pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini.


Kocha Ndayiragije aungana na Haji Manara
CORONA: Fabregas atoa sadaka mshahara wake