Jumla ya Wanawake 349 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia Mkoani Iringa, huku upande wa Wanaume waliokumbwa na kadhia kama hiyo wakiwa ni 49 kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2023.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Iringa, Allan Bukumbi wakati akizungumza na Askari wa kike Mkoani hapo Novemba 28, 2023 katika utelekezaji wa kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia yenye kauli mbiu isemyo “Wekeza kuzuia ukatili wa kijinsia” iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii na Dawati la Jinsia na watoto.
Amesema, takwimu zinaonyesha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha matukio kwa Wanawake na Watoto hivyo Jeshi la Polisi linapambana kutokomeza vitendo hivyo vinavyosababishwa na uelewa mdogo, mila potofu, ulevi, imani za kishirikina pamoja na migogoro ya kifamilia.
Aidha, amewataka Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoani Iringa (TPF – Net Iringa) kuwa mfano mzuri kwenye jamii na kupambana na vitendo hivyo vya ukatili kwa wanawake na watoto pamoja na kuwa na umoja na ushirikiano.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la jinsia na watoto Iringa, Mkaguzi wa Polisi Elizabeth Swai amesema kesi za ukatili wa kijinsia mara nyingi hutokea kwa watu wa karibu ambapo changamoto kubwa ni kwa wanandugu kutotoa ushirikiano kwa Polisi na kuanza usuluhishi baina yao, jambo linalopelekea kurudisha nyuma jitihada za kupambana na ukatili wa kijinsia.