Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amesema magaidi zaidi ya 300 kutoka msumbiji walivamia kijiji cha Kitaya Mkoani Mtwara na kufanya uharibifu na mauaji.
IGP Sirro ameeleza kuwa baadhi ya watu wamekamatwa ambapo kati yao baadhi ni raia wa Tanzania na wengine waliofanya mauaji na kurudi Msumbiji nao wamekamatwa.
“Ni kweli Wiki iliyopita, Magaidi wapatao 300 walitoka Msumbiji walivamia kituo chetu pale Kijiji chetu cha Kitaya (Mtwara), walifanya uhalifu mbalimbali na walifanya mauaji, tumefuatilia na baadhi ya watuhumiwa kadhaa, siwezi kuwataja wamekamatwa kuhusika na hayo matukio ambao wengine ni wa kwetu hapa walishirikiana na wengine kutoka nje”
“Ukifanya uhalifu Tanzania na damu ya Mtanzania haiwezi kwenda hivi, tunaendelea kupambana nao ili kuupata mtandao wote ulioanza kule Kibiti na Rufiji ambao tulipambana nao wakaona wameshindwa,” amesema IGP Sirro.
“Watanzania waelewe huu ni mtandao ambao ulianzia Rufiji, Kibiti wengine tulipambana nao wakaona wameshindwa wakakimbilia Msumbiji, kule wameungana na wenzao wanajaribu kurudi nyumbani, tumejipanga kuwa wakirudi tutawashughulikia na hata wakibaki huko tutashirikiana na wenzetu kuhakikisha hawatokuwa salama”
IGP Sirro ameongeza watahakikisha wanawakamata wahalifu na kuwapeleka mahakamani ili haki itendeke na kutoa rai kwa vijana wasijiunge kwenye makundi ya uhalifu.