Meneja wa Klabu bingwa Barani Ulaya Manchester City Pep Guardiola amekiri kuwa yuko tayari kupambana kumbakisha Kiungo kutoka Ujerumani Ilkay Gundogan katika Klabu hiyo zaidi ya msimu huu.
Mkataba wa sasa wa Gundogan katika Klabu ya City unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Juni, hii baada ya msimu wa kihistoria kwa mchezaji huyo na klabu, lakini FC Barcelona wametoa ofa kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, ili akacheza kule Camp Nou.
Guardiola hivi majuzi alifichua kwamba Mkurugenzi wa Michezo, Txiki Begiristain, anafanyia kazi mkataba mpya wa mchezaji huyo, lakini licha ya jitihada zao nzuri, inaelezwa kuwa FC Barcelona kwa muda mrefu wamekuwa na uhakika wa kupata huduma yake msimu huu wa majira ya joto.
FC Barcelona wamempa Gundogan mkataba wa miaka miwili pale Camp Nou, pamoja na chaguo la mwaka mmoja zaidi.
Vyanzo vya habari pia vimethibitisha kuwa familia ya mchezaji huyo inataka kuishi Hispania.
Hata hivyo, Guardiola hayuko tayari kukubali kushindwa kwa sasa na aliapa kupigana vita kumzuia nahodha huyo wa City kuondoka.
“Tuna nia ya kuongeza mkataba wake, lakini FC Barcelona nao wana nia ya kumsajili,” amesema Guardiola katika mashindano ya Gofu ya Puma Legends.
“Natumaini atabaki na sisi, bado tunapigania abaki. Ni mchezaji tunayetaka abaki, na tutafanya kila tuwezalo, lakini tunajua Barca wanamtaka.
Gundogan ni mmoja wa wachezaji kadhaa wa City wanaohusishwa na kuondoka pale kwenye Dimba la Etihad msimu huu wa majira ya joto, huku Bernardo Silva pia akitafuta kuondoka katika klabu hiyo msimu huu.