Jeshi la Israel limefyatua makombora kadhaa kuelekea eneo la Gaza, Palestina ikilenga wapiganaji wa kundi la Hamas.
Jeshi hilo la Israel limeeleza kuwa katika mashambulizi hayo lilipiga maeneo ya viwanda vya uzalishaji wa silaha na maghala ya silaha ya Hamas, mapema leo. Hata hivyo, kwa mujibu wa Independent, makombora hayo yalileta madhara katika maeneo ya makazi yakigusa pia watoto.
Hamaki kati ya Israel na Palestina iliongezeka wiki iliyopita baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Israel imekuwa ikidai Jerusalem ni mji wake mkuu wakati Wapalestina wakiendelea kudai upande wa Mashariki mwa mji huo kuwa eneo lao muhimu lililotwaliwa na Israel katika vita ya mwaka 1967.
Jana, kiongozi wa Hamas, Fathi Hammad alisema kuwa Taifa lolote litakalohamishia ubalozi wake Jerusalem litakuwa ‘adui wa Wapalestina’.
Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Augustine Maige imeweka wazi msimamo wake kuwa haitahamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem.
“Hatuna ulazima wa kuhamisha ubalozi wetu. Unapaswa kufahamu kuwa ubalozi wa Tanzania nchini Israel utabaki kuwa Tel Aviv na hakuna mpango wa kuuhamishia Jerusalem ingawa kumekuwa na jitihada za kutushawishi kufanya hivyo,” Waziri Maige anakaririwa na The Citizen.
Uamuzi wa Trump umepokelewa kwa hisia tofauti na mataifa mengi huku ikielezwa wazi kuwa utakwamisha mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.