Israel imeitisha uchaguzi mwezi Machi 2021 baada ya Bunge kushindwa kuidhinisha bajeti ya serikali ikiwa ndiyo muda wa mwisho uliopangwa kufanya hivyo.
Kushindwa kuidhinishwa bajeti kunaiporomosha serikali ya sasa ya muungano ya Israeli, iliyoundwa kati ya chama cha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na mpinzani wake mkuu, Benny Gantz, mnamo mwezi Mei, ili kupambana na changamoto za janga la virusi vya corona.
Kampeni za uchaguzi wa nne wa Bunge ndani ya miaka miwili, zitafanyika wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiwa anakabiliwa na changamoto kadhaa.
Miongoni mwao ni hasira ya umma inayotokana na jinsi alivyoshindwa kukabiliana na janga la virusi vya corona, huku akiwa katikati ya kesi ya ufisadi, ya kwanza dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel.
Mpinzani mkuu wa Netanyahu katika uchaguzi ujao ni Gideon Saar, Utafiti wa maoni ya raia kabla ya uchaguzi unaonyesha kuwa Saar anamkaribia sana Netanyahu kwa umaarufu miongoni mwa wapiga kura.