Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo ametaja mikoa ambayo haifanyi vizuri katika zoezi la uandikishaji wapigakura kwaajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Amesema atamuomba Rais John Magufuli aridhie viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao maeneo yao yatashindwa kuandikisha kwa asilimia 50 ya wapigakura wachukuliwe hatua kali.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya uandikishaji wa wapigakura, Jafo amesema tangu kuanza kwa uandikishaji Oktoba 8 hadi 14 mwaka huu baadhi ya mikoa imefanya vibaya.

Ametaja mikoa mitatu ambayo imefanya vibaya mpaka sasa ni Dar es salaam, unaoongozwa na Paul Makonda, ambao umefanikisha kwa asilimia 8, Kilimanjaro unaioongozwa na Anna Mghwira kwa asilimia 12, na Arusha unaoongozwa na Mrisho Gambo kwa asilimia 13.

Jaffo amesisitiza kuwa atampelekea Rais Magufuli dokezo kwa mikoa itakayoshindwa kufanya vizuri katika uandikishaji wapigakura katika uchaguzi huo ili achukue hatua.

Aidha Jafo amesema, wapo wakuu wa mikoa wanaoweza kuhamasisha watu kujaa uwanjani siku ya mechi za mpira ila suala la kujiandikisha wapigakura wanasuasua.

Ametaja mikoa ambayo imefanya vizuri kwa kujiandikisha zaidi ya asilimia 53 ni Iringa, Songwe, Mbeya na Tanga, na hadi sasa jumla ya watu milioni 5.8 wamejiandikisha.

Zaidi ya wananchi milioni 20 wantarajiwa kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.

 

Makala: Muasisi wa Tuzo za Nobel, ‘mfanyabiashara wa vifo’ alivyourudia ubinadamu
UWT yasisitiza madaraka 50 kwa 50