Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri, kukataa kutoa vibali kwa walimu na kuagiza wakurugenzi hao kutoa maelezo ni kwanini wanashindwa kutekeleza jukumu hilo.
Waziri Jafo ametoa kauli hiyo leo Desemba 21, 2020, kwenye mkutano wa 15 wa jumuiya ya wakuu wa shule nchini, ambapo ameeleza kuwa kwa mwaka 2020, walimu wamefanya kazi kubwa na kusaidia ongezeko la ufaulu na hivyo serikali imetenga fedha kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu.
Aidha amesema kuwa serikali inafanya kazi kubwa ya kutengeneza mazingira wezeshi kwa walimu huku lengo likiwa ni la kupunguza idadi ya watu wasio na elimu nchini.
Awali akizungumza kwa niaba ya wakuu wa shule Rais wa TAHOSA, Frank Mahenge, ameeleza changamoto ambazo bado zipo kwa walimu na shule za sekondari nchini na kutoa ombi kwa serikali kuweza kuzitatua.