Mwakilishi wa Mchezaji Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ Jasmine Razack amesema ataendelea kumpigania mchezaji huyo katika kesi ya kuvunja mkataba na Young Africans, ambayo ipo mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’.
Akizungumza na Clouds FM kwenye kipindi cha Sports Extra Jasmin amesema kinachotakiwa kufahamika kwa wadau wengi wa soka ni kujua Feisal Salum ana haki ya kuvunja mkataba na Young Africans na asichukuliwe kama mtu anayevuruga hali ya hewa klabuni hapo.
“Mkataba wa mchezaji unavunjika wakati wowote, AWE na SABABU au ASIWE na SABABU, hii ni haki ya mchezaji, weka mkataba pembeni ni haki yake.”
“Ukiwa na mkataba utasema umevunja kwa sababu ipi hata kama huna sababu, makubaliano ya pande mbili yataangaliwa lakini kumrudisha mchezaji akatumikie mkataba wake hairuhusiwi” amesema Jasmin
Hata hivyo Mkurugenzi wa Sheria klabu ya Young Africans Simon Patrick amesema: “Hatumng’ang’anii Feisal lakini tunataka utaratibu ufuatwe. Kama tutaruhusu Feisal kuondoka kwa njia hii, kuna siku hatutakuwa na mpira maana mchezaji ataamka asubuhi na atasema hana furaha basi anaondoka”
“Huu ni uhuni ambao hautakiwi kuruhusiwa katika mpira. Ziko njia rasmi za kuvunja mkataba na zinafahamika hadi (FIFA)”
“Tunachotaka kanuni za mpira zisimamiwe, tusiruhusu MAHARAMIA wanaotumia fedha. Ikitokea wameruhusu hili nina hakika kabla msimu haujaisha atatokea mwenye fedha atawajaza Mamillioni atawaambia andikeni barua hamna furaha poteeni baadae mtaomba kuvunja mikataba mtaruhusiwa. Na hii sio kwa Yanga tu klabu zote”
“Sisi tunachokitaka sheria na taratibu zifuatwe, sisi hatuwezi kumruhusu aondoke kiholela japo sio kwamba tunamng’ang’ania. Akifuata Utaratibu TUTAMRUHUSU AONDOKE, Yanga ni kubwa kuliko mtu yeyote”