Mshambuliaji wa Kimataifa wa DR Congo Jean Baleke amethibitisha kufanya mazungumzo binafsi na Uongozi wa Simba SC, na kilichobakia kwa sasa ni Klabu ya hiyo ya Msimbazi kumalizana na TP Mazembe.
Simba SC inahusishwa kumuwania Mshambuliaji huyo anayecheza kwa mkopo katika Klabu ya Nejmeh ya Lebanon akitokea TP Mazembe mwanzoni mwa msimu huu 2022/23.
Baleke amesema kwa sasa yupo mjini Kinshasa-DR Congo kwa ajili ya kufuatilia suala la uhamisho wake, lakini hatakuwa na maamuzi yoyote hadi Klabu za Simba SC na TP Mazembe zitakapofikia makubaliano.
“Nimewasili Kinshasa Jumanne kwa ajili ya mchakato wa suala langu la kusajiliwa na Simba ambayo iko tayari kuninunua lakini wenyewe TP Mazembe wanataka kunitoa kwa mkopo”
“Kama watakubaliana viongozi wa pande hizo mbili muda wowote kuanza wakati huu nitakuja huko Tanzania kwa ajili ya kujiunga na Simba ili kuanza kazi kwenye majukumu yangu mapya.” amesema Jean Baleke
Hata hivyo taarifa zinadai kuwa Klabu ya Simba SC inatia ngumu kumsajili Kwa Mkopo Mshambuliaji huyo kutoka TP Mazembe kwa kuhofia kuwa anaweza kufanya vyema katika kipindi cha msimu kilichosalia, hivyo klabu hiyo ikajikuta inampoteza akiwa kama Mchezaji huru.
Kwa mantiki hiyo Uongozi wa Simba SC unalazimisha uwepo wa kipengele cha kumsajili moja kwa moja mwishoni mwa msimu huu, endapo ataonyesha kiwango kizuri.
Kama mpango huo utashindikana Simba SC inaweza kuachana na Dili hilo, kisha kuhamia kwa Mshambuliaji mwingine Mkongomani, Jean Mundele Makusu ambaye ni Mchezaji huru kwa sasa.
Makusu ndio chaguo la Pili kwenye orodha ya Simba SC kupitia Dirisha Dogo la Usajili Kwa upande wa Washambuliaji.
Makusu tayari ameshavunja mkataba na Klabu ya FC Lupopo ya nchini kwao DR Congo, kufuatia sintofahamu zilizoibuka kati yake na Uongozi wa Klabu hiyo.