Klabu za Chelsea na Arsenal zinaendelea na vita ya kumuwania kiungo wa klabu ya Nice ya Ufaransa Jean-Michael Seri.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa mapema hii leo na kituo cha televisheni cha Sky Sports zimeeleza kuwa, uongozi wa klabu ya Chelsea haujakatishwa tamaa na mpango wa kumsajili kiungo huyo, licha ya kuonyesha yupo tayari kuondoka na kutimkia kaskazini mwa jijini London.
Arsenal wamekua na matarajio makubwa ya kumsajili Seri baada ya mchezaji huyo kuonyesha mapenzi na klabu hiyo, itakayoongozwa na meneja mpya Unai Emery kuanzia msimu ujao wa ligi ya England.
Tayari uongozi wa Nice umeshatangaza milioni 35 kuwa ada rasmi ya uhamisho wa Seri, huku kuajiriwa kwa meneja mpya klabuni hapo Patrick Vieira kukianza kuhisiwa huenda ikawa rahisi kwa The Gunners kumnyakua kiungo huyo, tofauti na ilivyo kwa Chelsea.
Hata hivyo pamoja na fununu hizo, bado mchezaji huyo yupo sokoni na huenda mwenye dau kubwa akafanikiwa kumchukua kwa urahisi katika kipindi hiki cha usajili barani Ulaya.
Seri mwenye umri wa miaka 26, ni raia wa Ivory Coast, na mpaka sasa ameshaitumikia klabu ya Nice katika michezo 101 na kufunga mabao 11.
Alisajiliwa klabuni hapo mwaka 2015 akitokea nchini Ureno alipokua akiitumikia klabu ya Paços de Ferreira.