Waziri wa Ulinzi wa Malaysia, Hishammuddin Hussein amesema kuwa uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem (Yerusalem) kama makao makuu ya Israel ni kama kofi kwenye sura ya dunia ya Uislam.
Hussein aliongeza kuwa jeshi la nchi hiyo liko tayari likisubiri maelekezo kufanya kazi kuisaidia Palestina kwa namna yoyote.
“Tumekuwa tunajiandaa kwa lolote linaloweza kutokea. Jeshi letu liko tayari wakati wote likisubiri maelekezo kutoka kwenye uongozi wa juu,” Hussein anakaririwa na shirika la habari la Malaysia la Bernama.
Aliongeza kuwa nchi hiyo inaomba mgogoro huo usipelekee mvurugano zaidi.
Uamuzi wa Trump umesababisha kufanyika kwa maandamano makubwa ya kuupinga katika nchi za Uturuki, Misri, Jordan, Tunisia, Algeria, Iraq na nyingine hasa za kiarabu.
Mapema leo, zaidi ya watu 10,000 waliandamana na kufika nje ya ubalozi wa Marekani nchini Indonesia, wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali kama ‘Ubalozi wa Marekani Uondoke Al Quds’, ‘Tuko Pamoja na Wapalestina.
Al Quds jina la kiarabu kwa mji wa Jerusalem.
Kumekuwa na mgogoro kati ya Palestina na Israel kuhusu umiliki wa mji wa Jerusalem ambao pande zote zinadai zinaumiliki kihalali, huku Palestina ikiidai zaidi Mashariki ya Jerusalem.