Mabosi wasumbufu ni kitu cha kawaida Tanzania. ukiuliza kikundi cha wafanyakazi, ‘unaridhika na bosi wako?’, litakuwa si jambo la kushangaza wengi wao watakapo kujibu, ‘hapana’. Ingawa unaweza kufikiri kuwa wafanyakazi wengi hawapendi mabosi wao kwa sababu tu wanawapa kazi nyingi za kufanya na pale wanapokosea wanakemewa, lakini ukweli ni kwamba, wengi wetu haturidhishwi na mabosi wetu. Si kwa sababu ya kazi wanazotupa, bali sababu ya tabia zao.
Ni watu wachache sana Tanzania (na duniani kote) ambao wamepata bahati ya kufanya kazi na mabosi wanaoridhika nao, na mara nyingi inabidi uvumilie kejeli, dharau na maamuzi yasiyo ya haki pamoja na kuishi kwa uoga wa wasimamizi wako. Bahati mbaya, mabosi wabaya ni kitu cha kawaida, na kibaya zaidi ni kuwa wafanyakazi wengi wanahisi kuwa hawana nguvu ya kushindana nao, hivyo hukaa kwenye mazingira ya kazi magumu sababu tu wanahitaji ajira. Na pale wanaposhindwa kabisa, huacha kazi.
Nini hasa kinacho fanya Bosi awe mbaya?
Kuna sababu nyingi zinazoweza kumfanya mtu awe meneja, msimamizi, kiongozi wa timu au CEO mbaya. Lakini, sababu za muhimu zaidi ambazo zinaweza kuingilia utendaji kazi wako ni:
- Wana chukua sifa za kazi ulizofanya wewe, bila kuonyesha mchango wako
- Wana dharau na kuongea na wewe kwa kejeli na kufoka
- Wana kuwekea malengo ya kazi ambayo hayafikiki
Kama bosi wako ana moja au zaidi ya tabia hizi, basi ni bosi mbaya. Lakini, usikate tamaa, kuna njia za kushughulika na bosi msumbufu ili uweze kuendelea kupenda kazi yako. Na hizi hazihusishi kuwapiga makofi ya uso au kuwarushia meza — hizi njia zibaki kwenye ndoto tu.
- Elewa nini kimesababisha wawe hivyo
Njia nzuri ya kushughulika na bosi wako, kwanza jua nini kinawakera. Tabia yao mbaya inaweza kusababishwa na:
- Kuzidiwa na kazi
- Wanahisi hawajitoshelezi katika nafasi waliyopo, ingawa mabosi wengi wana ujuzi katika fani zao, yawezekana kuwa hawajapata mafunzo ya uongozi bora.
- Wanapenda kujigamba
- Hawawezi kuwasilisha mawazo yao vizuri
- Wanapenda kujionyesha wako juu kwa watu wengine kwa kukukejeli wewe
Kwa ufupi, unatakiwa ujue kuwa tabia mbaya ya bosi wako haisababishwi na wewe. Na ukishajua hili basi utakua na mwitikio tofauti pale watakapo kukera.
Kwa mfano, mteja hajaridhika na kazi uliyofanya na badala ya bosi wako kukurekebisha na kukueleza nini unatakiwa uboreshe, anaanza kufoka na kulita jina lako. Ukishajua kuwa tabia yao inasababishwa na imani yao kuwa hofu inamfanya mfanyakazi afanye kazi kwa bidii zaidi, badala ya usikivu na ufundishaji basi atakapokufokea haitakukera sana wala kuvunja ujasiri wako. Hata hivyo, ingawa unatakiwa ukubali pale unapofanya kosa, usikubali dharau kama njia ya adhabu.
- Ongea na Bosi wako
Ingawa unaweza ona kuwa kukaa kimya au kulalamika kwa wafanyakazi wenzako ndio njia rahisi, ni vizuri zaidi na itakusaidia ukiongea na bosi wako. Kwanza unatakiwa ujue, kuongea na bosi wako kuhusu tabia yake sio sababu ya kufukuzwa kazi. Na kama bosi wako akijaribu kukutishia hivyo, basi mshitaki kwa Afisa Rasilimali Watu (HR). Kwa bahati nzuri, sheria za Tanzania zinamlinda zaidi mwajiriwa kuliko mwajiri, na hivyo inakuwa ngumu kumfukuza kazi mfanyakazi aliyeajiriwa kikamilifu.
Lakini hata kama sheria inakulinda, hii isiwe sababu ya wewe kuongea na bosi wako kwa kejeli. Badala yake tafuta njia ya busara ya kuwasilisha malalamiko yako kwake. Usingependa waanze kujitetea kabla hawajakusikiliza hivyo badala ya kusema kitu kama “Sipendi unavyonifokea, unanivunjia heshima”, elezea shida zako katika namna nzuri kama, “Napenda kufanya kazi na wewe, lakini pale unapoongea na mimi kwa kufoka unanifanya nijisikie vibaya na hivyo kushusha utendaji wangu”.
Pia, pamoja na kuonyesha ni jinsi gani tabia ya bosi wako inakuumiza wewe, onyesha pia ni jinsi gani inaingilia utendaji wako na malengo ya bisahara kwa ujumla. Mfano “Wiki iliyopita, ulivyo niita mjinga mbele ya mteja, haukuniabisha tu, bali pia uliteteresha heshima ya mteja kwangu, na hivyo kuathiri biashara kiujumla”.
Mwisho, kumbuka kuwa mabosi wengi wabaya ni sababu hawana mafunzo au sababu wanapenda majigambo, hivyo ongezea kitu kama “Naelewa kuwa nimekosea kwenye kazi hii, na ninatumia juhudi zote kufanya marekebisho. Lakini pia, ningependa tuweze kuwasiliana vizuri ili kuboresha utendaji wa biashara. Hivyo, wewe unapendekeza tuendelee vipi?” Hii inawafanya wasijitetee na badala yake wakusikilize sababu umekubali makosa yako, na unawaweka kwenye nafasi ya kuonekana wenye busara kwa kuwaomba ushauri wao.
2. Wafanye waonekane wenye bidii
Unaweza usifurahie kufanya hivi, na inawezekana kuwa tayari wanajisifia kwa kazi ulizofanya wewe, lakini kumfanya bosi wako aonekane ni mwenye bidii yaweza kua ndio jibu la matatizo kati yenu. Hili ni kweli hasa pale unapogundua kuwa chanzo cha tabia mbovu ya bosi wako ni sababu hajiamini. Ukishajifunza udhaifu wake, mfano siku zote anachelewa kwenye mikutano, au kuna programu ya kompyuta ambayo inamsumbua kutumia, au hawezi kuongea na wateja vizuri – msaidie kufanya haya na mwache ajisifie kuwa amefanya mwenyewe.
Bosi wako anaweza asikushukuru wazi, lakini kwa kumuacha ajisifie kwa kazi ulizofanya wewe utamuonyesha kuwa anakuhitaji. Na akishagundua hili, basi atajirekebisha tabia yake ili muweze kuelewana.
Lakini, inabidi kuwe na ukomo kwenye vitu ambavyo utafanya bila bosi wako kutambua mchango wako au kukulipa. Mfano pale unapofanya kazi zao katika muda wako binafsi, au unapomsaidia kuleta mteja halafu hakupi sehemu ya kamisheni, usikubali.
3. Wasilisha matatizo yako kwa HR
Pamoja na kuongea na bosi wako, kama asipobadilika, wasilisha malalamiko yako kwa HR. Ni wajibu wa idara ya HR kuhakikisha mahala pa kazi ni sehemu salama kwa wafanyakazi wote, hivyo usiogope kumshtaki bosi wako. Zaidi, usiongee tu kwa mdomo na HR, tuma barua pepe, weka rekodi ya maandishi ya malalamiko yako. Hii itakusaidia kama utafukuzwa kazi kimakosa, au kama itatokea sababu ya kukufanya uchukue hatua za kisheria.
4. Jua ukomo wako
Kila mtu ana ukomo wake wa kukubali kero, sio vizuri kuufikia. Hivyo kama umejaribu kutatua matatizo yaliyopo na imeshindikana, na hautaki kuchukua hatua za kisheria, basi ni wakati wa kutafuta kazi mahala pengine. Unaweza fikiri kuwa ukiacha kazi bosi wako anakuwa ameshinda, lakini ukweli ni kwamba unatakiwa uangalie afya yako ya kiakili na ya kimwili. Hivyo inapofikia mahala unaona hasara za kufanya kazi na bosi wako ni kubwa kuliko faida, basi ni muda wa kuacha kazi.
5. Chagua kazi vizuri
Ukiamua kuondoka kwenye kazi uliyopo sasa, hakikisha unafanya uchunguzi wa kina kuhusu atakaye kuwa bosi wako mpya kabla hujakubali ofa ya kazi. Ongea na watu waliowahi kufanya nao kazi, ongea na wafanyakazi wao wa sasa na wadau wengine wanomjua katika fani hiyo. Pia wakati wa mahojiano, mchunguze tabia yake kwa maswali kama ‘aina ya uongozi wako ikoje?’, ‘kwanini mfanyakazi aliyekuwepo kabla yangu aliondoka?’. Angalia jinsi anavyo ongea na wafanyakazi wengine. Hii itakusaidia kuongeza nafasi ya kupata bosi utakae ridhika nae.
Mabosi wabaya ni wafanyakazi ambao hawajapata mafunzo
Umeshwawahi kusikia msemo wa, ‘kila mtu ana bosi wake’? Ingawa waweza kuona kuwa bosi wako ndio mtu mkuu zaidi ofisini, mara nyingi si kweli isipokuwa kama alianzisha kampuni mwenyewe au anamiliki sehemu kubwa zaidi ya kampuni, kama si hivi basi naye lazima aliajiriwa na anaweza kubadilishwa. Hivyo kama umefanya kila kitu, pamoja na kuwasilisha malalamiko yako kwa HR lakini hakuna kilichobadilika, basi ni muda wa kuongea na bosi wake.
Kukutana na uongozi wa juu ili kuongea nao kuhusu tabia za bosi wako ni jambo la kuogopesha, lakini kama una ushahidi wa maandishi wa malalamiko yako na msaada kutoka kwa wafanyakazi wenzako, basi utakuwa na kesi nzuri. Hawawezi kukufukuza, hivyo usiogope. Lakini kama uongozi wa juu usipochukua hatua yoyote kurekebisha tabia ya bosi wako, kama kumtaka kuchukua mafunzo ya uongozi, basi ni bora uanze kutafuta kazi nyingine.
Mwisho wa siku, maisha ni mafupi mno kufanya kazi na bosi msumbufu.