Dakika chache baada ya kukamilisha taratibu za kujiunga na Klabu ya Arsenal akitokea Chelsea, Kiungo kutoka nchini Italia Jorge Luiz Frello Filho ‘Jorginho’, amefichua siri kubwa kwa kusema, Klabu hiyo ya Kaskazini mwa jijini London ilijaribu kumsajili mara kadhaa lakini ilishindikana.
The Gunners wamekamilisha uhamisho wa kiungo huyo jana Jumanne (Januari 31), kabla ya kufungwa kwa Dirisha Dogo la Usajili, kwa ada ya Pauni Milioni 12.
Meneja wa Arsenal Mikel Arteta alipendekeza kusajiliwa na kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31, ili kuziba nafasi ya Kiungo wa Misri Mohamed Elneny anayeuguza jeraha kubwa la goti.
Jorginho amezungumza kupitia Tovuti ya Arsenal na kueleza shauku yake baada ya kusajiliwa na Klabu hiyo, huku akifichua siri namna mpango wa kuhamia klabuni hapo ulivyoshindikana siku za nyuma.
“Alikuwa na ushawishi mkubwa kwa sababu nafahamu alijaribu mara chache kunipata, lakini haikuwezekana kwa sababu kadhaa, sio kwa matakwa yangu. Kwa hivyo bila shaka, alikuwa na matarajio makubwa dhidi yangu,” Jorginho aliambia tovuti rasmi ya Arsenal.
“Nimefurahishwa sana na changamoto hii mpya, na siwezi kungoja kuwa uwanjani! Kila kitu kimetokea haraka sana. Nilishangaa kidogo, lakini nilichukua fursa ya changamoto hii ya ajabu. Ni klabu ya ajabu, kubwa, na ninafurahia kuwa hapa.”
Arteta alisema: “Jorginho ni mchezaji mzuri na mwenye akili kubwa, ujuzi wa kina anapocheza eneo la kiungo, kiasi kikubwa cha uzoefu wa Ligi Kuu na Michezo ya kimataifa.”
“Jorginho amekuwa na mafanikio makubwa katika historia yake, lakini bado ana njaa na nia kubwa ya kufanya jambo akiwa na wachezaji wengine hapa. Tumefurahi sana kumsajili Jorginho na kumkaribisha yeye na familia yake kwenye klabu.”
Naye Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal Edu aliongeza: “Jorginho ni mtaalamu aliyeimarika na mwenye akili timamu ambaye analeta ubora na uzoefu katika kikosi chetu. Ni mchezaji anayelingana na mtindo wetu wa uchezaji, na anajiunga nasi katika wakati mzuri sana ambapo anaweza kuchangia katika nafasi muhimu ya kusaidia kudumisha kasi yetu.
Jorginho anatarajia kujiunga na kikosi cha Arsenal leo Jumatano (Februari Mosi), tayari kwa maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya ENgland, ambapo The Gunners itapapatuana na Everton mwishoni mwa juma hili.