Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watendaji wa kata nchini kutambua kuwa wao ndio wasimamizi wa kata zao na wanapaswa kuwawajibisha Wakuu wa Mikoa na hata Mawaziri wanapokiuka misingi ya utawala bora kwenye kata zao.
Akizungumza leo kwenye mkutano na watendaji hao wa kata kutoka mikoa yote nchini, uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amewaeleza kuwa wanapoona mtendaji wa ngazi za juu anaenda kinyume na misingi ya utawala bora wanapaswa ‘kumlima barua’ na kutuma nakala kwa ofisi ya Rais.
“Kwenye kata yako kuna Mkurugenzi, Mkuu wa Mkoa au hata Waziri… wewe mtendaji wa kata ndio msimamizi. Hata kama kuna kiongozi wa nafasi gani yuko chini yako na anapoonekana anaenda visivyo unapaswa kumuwajibisha au kutoa taarifa kwa mamlaka yake,” amesema Rais Magufuli.
“Unaweza kumuandikia maoni, na usiogope hata kumlima barua hata kama anakuzidi cheo, eleza kwamba katika kata hii naona mtumishi huyu anakwenda kinyume na maadili, halafu nakala unapiga hapa kwangu. Ni lazima tujifunze kuogopana,” ameongeza Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewataka watendaji hao kuhakikisha wanabeba kero za wananchi na kuzitatua bila kusubiri ziara za viongozi wa ngazi za juu.
Amesema watendaji wa kata ndio viongozi walio karibu zaidi na wananchi na pale wanapoona kero hizo ziko juu ya uwezo wao waziwasilishe kwa viongozi wa ngazi ya juu.
Amewakumbusha kusimamia maelekezo ya Serikali katika masuala mbalimbali kama kufuta tozo za mazao chini ya tani moja pamoja na tozo nyingine zaidi ya 80 kwenye sekta ya kilimo na uvuvi.