Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) Dkt. Anna Makakala, amefanya ziara ya kushitukiza katika Uwanja wa ndege wa kimatifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam na kufanya ukaguzi wa pasipoti kwa wageni na raia waliowasili uwanjani hapo kwa ndege ya Shirika la Ethiopia.
Makakala amefika uwanjani hapo ikiwa ni moja ya ziara zake za kikazi ambapo hutembelea mipaka na vituo vya uhamiaji nchini, kufanya ukaguzi wa mipaka na kukagua utendaji kazi wa maafisa na askari wa Uhamiaji katika maeneo yao ya kazi.
Amesema Tanzania imepakana na nchi takriban nane zenye mipaka mikubwa na vituo vya kutolea huduma za kiuhamiaji zaidi ya 80 hivyo ni vyema wageni wote na raia wa Tanzania kutumia utaratibu wa kuingia na nchini kupitia njia halali zilizorasimishwa kwa njia halali.
“Tupo kwenye kipindi cha uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani ni lazima tuhakikishe tunaumaliza uchaguzi wetu salama, lakini pia tumeongeza nguvu mipakani na kufanya doria na misako ya mara kwa mara ili kuilinda nchi yetu, nawaomba sana Watanzani tushirikiane katika kuilinda mipaka yetu kwani jukumu la ulinzi na usalama wa nchi yetu ni letu sote”. amesema Makakala.